Yanga SC

MECHI YA AZAM FC YABEBA HATMA YA MSIMU WA YANGA

Vardo June 23, 2026 11:28 am

MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kwa sasa nguvu zote za klabu hiyo zimeelekezwa katika michezo mitatu iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha timu inamaliza msimu kwa mafanikio na kutetea ubingwa wake.

Kamwe amesema kila mchezo uliobaki una umuhimu mkubwa kwa Yanga na hakuna nafasi ya kufanya makosa, kwani kupoteza pointi katika hatua hii ya mwisho kunaweza kuathiri malengo yao ya kutwaa taji la ligi.

Ameeleza kuwa ndani ya kikosi hicho kuna uelewa wa pamoja kuhusu uzito wa mechi zilizobaki, jambo ambalo limewafanya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kuendelea kushikamana kuelekea katika hatua ya mwisho ya msimu.

“Tunatakiwa kushikamana kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo hii iliyosalia. Tutaumia sana tukiangusha pointi na kupoteza ubingwa,” ameema Kamwe.

Msemaji huyo alibainisha kuwa mchezo wao ujao dhidi ya Azam FC utakuwa wa muhimu sana katika mbio za ubingwa, hivyo maandalizi yote yanafanyika kwa umakini mkubwa ili kupata matokeo chanya.

Kamwe amesema baada ya mchezo huo dhidi ya Azam FC, uongozi wa klabu utaanza kufanya tathmini ya kina kuhusu mwenendo wa timu katika msimu huu, ikiwemo mafanikio na changamoto zilizojitokeza.

“Tunacheza na Azam FC Jumatano, baada ya hapo tutafanya tathmini ya timu yetu kuangalia nini tumefanya msimu huu hadi hapo tulipofikia,” amesema Kamwe.

Kauli hiyo inaonyesha wazi kuwa Yanga imeweka mkazo katika kumaliza kwanza majukumu ya uwanjani kabla ya kuanza mchakato wa kutathmini safari yao ya msimu wa 2025/26.

TPBRC YAGUSA KILIO CHA MABONDIA SIMBA YATAMKA WAZI KIKWAZO KIKUBWA NI AZAM FC