Michezo Bongo

TPBRC YAGUSA KILIO CHA MABONDIA

Vardo June 23, 2026 8:32 am

WAKATI mabondia na wadau wa mchezo wa masumbwi nchini wakitoa kilio cha gharama kubwa za vipimo vya MRI/CT Scan, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imesema imeanza kushughulikia suala hilo kwa kutafuta udhamini na hospitali.

Katika uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, wadau wa ngumi wanaeleza kuwa gharama kubwa za vipimo vya MRI na CT Scan zinawafanya mabondia wengi kushindwa kuvifanya, jambo linaloweka maisha yao hatarini.

Wanasema baadhi ya mabondia huingia ulingoni wakiwa na majeraha yaliyofichika na baadaye hupata ulemavu au kupoteza maisha baada ya kupigwa. Wameiomba Serikali, wadhamini na mamlaka za ngumi kupunguza gharama za vipimo, kuboresha upatikanaji wa bima na kuimarisha usimamizi wa uchunguzi wa afya ili kulinda maisha ya mabondia.

Hayo yakibainishwa, Kanuni za Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) za mwaka 2024, zinasisitiza umuhimu wa kila bondia kupima kabla na baada ya pambano, lakini hakuna ulazima wa kipimo cha MRI/CT Scan.

Kanuni 4.1.2 inasema siku 14 kabla ya kushiriki pambano lolote la ngumi za kulipwa bondia atawajibika kupimwa afya yake na daktari mwenye leseni ya kamisheni na anayetambulika na Chama cha Madaktari wa tiba za michezo (TASMA).

Kutokana na majibu ya vipimo daktari atashauri iwapo bondia husika anaweza au hawezi kushiriki pambano.

Kanuni za kimataifa za ngumi zinahitaji mabondia kufanyiwa uchunguzi wa afya, huku MRI au CT Scan ya ubongo ikihitajika katika mazingira maalumu au kwa vipindi vinavyowekwa na shirikisho au mamlaka husika; si lazima kabla ya kila pambano.

Mfano, Shirikisho la Kimataifa la Ngumi (IBA), lililokuwa likijulikana awali kama AIBA katika kanuni zake zilizoboreshwa MRI/CT Scan inapendekezwa kabla ya kushiriki mash indano makubwa kama mashindano ya dunia. Pia bondia akipigwa KO au TKO vipimo hivyo vitahitajika.

Kauli ya TPBRC

Makamu Mwenyekiti wa TPBRC, Jacob Mbuya, anasema wameingia udhamini na Hospitali Hitech Sai, iliyopo Upanga mkoani Dar es Salaam na kwamba, mabondia wanne wameshafanyiwa vipimo hivyo baada ya ushauri wa daktari.

“Uongozi uliopita ndio ulianza kufanya mazungumzo na hospitali hiyo, sisi tuliendeleza walipoishia kuhakikisha tunaanza kufanya nao kazi. Huko mbeleni bondia atakayepigwa KO ndiye atapimwa MRI/CT Scan,” anasema.

Mbuya anasema: “Zamani mabondia walikuwa hawapimi kutokana na gharama, baada ya kuona changamoto ni kubwa tuliomba udhamini wa hospotali hiyo.”

“Mambo yakiwa mazuri huko mbeleni tutakuwa na gym ambazo zina vipimo hivyo ili bondia apime kabla na baada ya pambano, kwa sasa itakuwa ngumu kwa hali halisi ilivyo,” anasema.

Rais mstaafu wa TPBRC, Chaurembo Palasa anasema hawakuweka mkazo wa moja kwa moja katika vipimo vya MRI/CT Scan isipokuwa bondia akipigwa KO atatakiwa kukaa nje miezi miwili hadi mitatu inategemea na ngumi aliyopigwa.

Anasema anaporejea kazini ni lazima atakuwa amepima vipimo hivyo kuonyesha usalama wa kichwa chake.

“Hatukusisitiza katika kanuni zetu (vipimo vya MRI/CT Scan) kwa sababu gharama ni kubwa, lakini bondia akipigwa KO lazima apumzike na kufanya vipimo hivyo. Katika ngumi utimamu wa afya ni kitu muhimu ndiyo maana mabondia wanapimwa mara kwa mara HIV, magonjwa ya ini na mengineyo,” anasema na kuongeza:

“Katika uongozi wangu sijawahi kuona bondia akawa kichaa, isip okuwa vifo vichache na magonjwa me ngine yanayotokana na ngumi, hayo yote wengi wao wanakuwa wamepigana uswahilini kwa sababu hawajapima na wanapopanda ulingoni inaibua matatizo ya nyuma.”

“Nashauri kungekuwa na bodi ya ngumi inayokuwa chini ya Serikali. Iwe kama ilivyo bodi ya filamu ambayo ipo chini ya Serikali, ndiyo maana wasanii wakikosea wanachukuliwa hatua za kisheria,” anasema.

Anasema uwepo wa bodi hiyo ya kisheria utasaidia kuufanya mchezo wa ngumi kuwa salama.

Palasa anasema mabadiliko ya katiba mpya yaliyofanyika anatarajia yatakuwa na mwanga mkubwa wa usalama wa mabondia.

“Mabadiliko yamefanyika bado kupitishwa, yakipitishwa yatakuwa na saini ya viongozi na muhuri kama unavyoona katika kanuni ambazo tulisaini sisi ambazo bado zinatumika hadi sasa hadi mpya zipitishwe,” anasema.

Anasema katiba ya kwanza iliundwa mwaka 2018 na mwaka 2019 ukafanyika uchaguzi lakini viongozi hawakumaliza muda wao.

Kauli za madaktari

Daktari wa ngumi nchini, Khadija Khamis anasema tatizo la mabondia kuanguka ulingoni siyo kila tukio ni la ghafla, mengine yanatokana na rekodi za nyuma.

“Mara nyingi ukiona bondia kapigwa panchi akaanguka ulingoni akipimwa anaonekana kovu la historia ya nyuma na ukimkuta na alama mpya za kipigo ndani ya kichwa basi panchi itakuwa ilikuwa kali sana,” anasema.

Dk Khamis anasema: “Vipo vitu vingi nje ya ngumi vinaweza vikasababisha makovu au kuvilia damu kichwani. Mfano, bondia kachelewa kurudi kwake na amelewa, mkewe kampiga na mwiko au sufuria akajisikia vibaya kisha akanywa dawa za kutuliza maumivu akajisikia vizuri, anapokuja katika pambano na amepima vipimo vya kawaida visivyoonyesha ndani ya kichwa, akipanda ulingoni akiguswa kidogo tu anazimia.”

Anasema vipimo vya MRI au CT Scan kwa hospitali za serikali ni takribani Sh800,000 na za binafsi ni Sh.1.5 milioni, gharama ambayo ni kubwa hivyo kuwa ngumu kwa mabondia kuzimudu.

Kupitia udhamini anasema waliweza kupima afya za mabondia, ambao wengi wao walipimwa MRI mara moja kwa mwaka.

“Katika katiba mpya ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania ambayo imepelekwa Baraza la Mic hezo Tanznia (B MT) ili ipitiwe na wanasheria, ndani yake kuna mambo mengi ya afya za mabondia. Tumeomba udhamini wa hospitali binafsi, wakimaliza kupitia na ikakubalika nadhani tutaanza utekelezaji,” anasema.

Dk Khamis anasema: “Kama hilo litapita basi makubaliano katika hospitali hiyo ni pamoja na kipimo cha MRI kutoka Sh1.5 milioni hadi Sh250,000 hiyo itakuwa ndani ya uwezo wao.”

Anasema mpango wao ni kutembelea kila gym ili kuzungumza na makocha, mapromota na mabondia kuhusu afya zao.

“Mfano bondia akilalamika kichwa lazima akapime kuliko kumeza panadol kisha anapoa, kumbe anaweza akawa na tatizo kubwa linaloweza likatokana na ngumi au maisha binafsi. Tunawaelimisha namna ya kula, kupangilia mlo, wanalala wapi, makocha kipi wakifanye kulinda afya za mabondia ni vitu vingi ambavyo vinalenga kulinda afya zao,” anasema.

Anamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuwapa bima za afya mabondia zitakazowasaidia kupunguza gharama hata kama haitatibu kila kitu.

Abel Shindika, daktari wa mpira wa miguu, anasema aliwahi kuwapokea mabondia wawili waliohitaji vipimo vya MRI na CT Scan lakini kwa kukosa pesa waliomba kuchomwa sindano za kuondoa maumivu kwa muda.

“Kipimo ni muhimu katika mwili wa binadamu, kwani kinaonyesha tatizo lipo wapi kisha litibiwe, ila gharama ndiyo changamoto kwa maelezo ya mgonjwa itabidi asaidiwe dawa ya maumivu isiyotibu,” anasema na kuongeza:

“Mabondia niliowahi kuwapokea walikuwa wanalalamika kichwa na kwa maelezo yao ilikuwa lazima wapime CT Scan ila hawakuwa na pesa. Walichofanya ni kuomba dawa za maumivu ya kutuliza, ila sikujua baada ya hapo kipi walikifanya ingawa niliwasisitiza watafute fedha wakapime,” anasema.

Kupitia Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (TASMA), anasema wamekuwa wakiomba gharama za vipimo hivyo ipungue.

“Hatuna pesa za kutibia wanamichezo wote ni wengi, maana kila mtu kaajiriwa sehemu yake. Nimewahi kushuhudia mabondia wanaoachana na mchezo huo kwa kukosa pesa za matibabu, wengine hata wadhamini wao hawana pesa,” anasema.

 

CHUGA FOUNTAIN  GATE NJIA NYEUPE YANGA