YANGA SC imepata pigo jipya baada ya mshambuliaji wake, Prince Dube, kushindwa kuungana na kikosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
Hii ni changamoto nyingine kwa timu inayokabiliwa na wimbi la majeruhi ndani ya kikosi chake.
Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amethibitisha kuwa Dube amelazimika kubaki Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya kina kufuatia kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya TRA FC uliochezwa jana.
Wakati Dube akiwa jijini chini ya uangalizi wa kitabibu, kikosi cha Yanga kimewasili Dodoma kujiandaa na mchezo ujao utakaopigwa Machi 21 katika Uwanja wa Jamhuri.
Ukosefu wa Dube ni pigo kubwa, kwani tayari baadhi ya wachezaji wakiwa nje kutokana na majeraha. Miongoni mwao ni Laurindo Aurelio ‘Depu’, Chadrack Boka, Ibrahim Bacca, na Edmund, wote wakikabiliwa na changamoto za kiafya. Hali hii inazidi kuipa benchi la ufundi changamoto kubwa katika kupanga kikosi imara.
Aidha, wachezaji wengine kama Dickson Job na Clement Mzize wanakabiliwa na majeraha ya muda mrefu, jambo linalohitaji mkakati makini kutoka kwa kocha na ufundi wa Yanga ili kuhakikisha timu inabaki yenye ushindani katika michezo ijayo.
Yanga inakaribia mchezo huu ikiwa na presha kubwa, baada ya kupata sare mbili mfululizo dhidi ya TRA FC na Azam FC, jambo linaloongeza dhiki ya kutafuta ushindi ili kudumisha nafasi ya kilele na kuendeleza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu.
Benchi la ufundi linapaswa kufanya maamuzi ya busara, huku mashabiki wakitarajia kikosi cha Yanga kuonyesha uthabiti na kushinda vikwazo vya majeruhi katika michezo ijayo, kuhakikisha kuwa timu inabaki mstari wa mbele katika mbio za ubingwa.