LICHA ya kukumbwa na wimbi la majeruhi kwa baadhi ya wachezaji muhimu, uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa bado una imani na kikosi chao, ukisisitiza kuwa kina uwezo wa kupata matokeo chanya katika michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema licha ya changamoto ya majeruhi, hawatakiwi kuyumba kwani wana kikosi kipana chenye uwezo wa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika kila mchezo, wakianzia na ule dhidi ya Mtibwa Sugar.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho Jumamosi kuvaana na wenyeji wao Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, ikiwa na lengo la kuondoka na alama tatu muhimu.
Kamwe ameweka wazi dhamira ya kikosi hicho kuelekea mchezo huo, akisisitiza kuwa lengo lao kuu ni kupata matokeo mazuri licha ya kutambua ugumu wa pambano hilo.
Amesema wapinzani wao wamekuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa, jambo linaloongeza ushindani uwanjani.
Ameongeza kuwa ndani ya kikosi hicho hakuna jambo linalopewa kipaumbele zaidi ya ushindi, huku akionyesha imani kubwa kwa wachezaji waliopo kuwa wako tayari kupambana hadi mwisho ili kuhakikisha wanapata alama tatu.
“Hatuna dhamira nyingine zaidi ya kushinda katika mchezo huo. Binafsi naamini tumeshavuka kipindi kigumu na sasa ni wakati wa kupata matokeo,” amesema Kamwe.
Aidha, amekumbushia uzoefu wa msimu uliopita ambapo walipoteza alama sita muhimu katika kipindi kama hiki dhidi ya Azam FC na Tabora United, hali iliyowaathiri kwenye mbio za ubingwa.
Kutokana na historia hiyo, Kamwe amesisitiza kuwa safari hii wamejipanga vizuri zaidi ili kuepuka makosa ya nyuma na kuhakikisha wanatumia kila nafasi wanayopata kuimarisha nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.