Home Habari za michezo SIMBA KUPELEKA KESI CAS NA FIFA KUFUATIA URAIA WA DAMARO

SIMBA KUPELEKA KESI CAS NA FIFA KUFUATIA URAIA WA DAMARO

0

UONGOZI wa klabu ya Simba umeweka wazi kuwa, licha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulitupia mbali ombi lao la kupata ufafanuzi juu ya uraia wa Mohammed Damaro, sasa wanaupeleka suala hilo kwa mashirika ya kimataifa ya mpira wa miguu, FIFA na CAS.

Simba ilipeleka maombi rasmi kwa TFF kutaka ufafanuzi kuhusu uraia pacha wa nyota huyo wa Yanga, jambo lililokuwa changamoto kwa klabu hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema tatizo la Damaro linahusiana na uraia wake na nafasi ya kucheza timu ya taifa.

“Tulikaa na kutafakari kwa kina, lakini jambo halijakaa sawa. Kuna klabu moja inatumia nafasi hiyo kuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya walioruhusiwa kikanuni. Mwaka jana sisi pia tuliandika barua ya kubadili uraia wa wachezaji wetu, lakini hatujajibiwa hadi leo,” amesema.

Magori ameongeza kuwa TFF haikuhakikisha uwiano sawa kati ya timu na mchezaji, jambo ambalo limepelekea Simba kupeleka malalamiko kwa CAS na FIFA.

“Hili japo sio tu tunakwenda CAS, bali pia tunaiandikia FIFA. Kama mtu anapewa uraia ili tu achezee klabu bila timu ya taifa, ni jambo lisilokubalika. Damaro hata ipite miaka 100 hawezi kucheza timu ya Taifa,” amesema .

Mwenyekiti huyo ameashiria kuwa tatizo hili si la kawaida, kwani kuna timu inayodai kuwa na wachezaji 13 kwa kutumia njia za mlango wa nyuma, jambo ambalo wanaliita udanganyifu mkubwa.

“Hili jambo sio fair. Kuna timu moja ina wachezaji 13 kwa kutumia mlango wa nyuma. Na aliyedanganya mamlaka kwamba anapewa uraia ili acheze timu ya taifa, alifanya udanganyifu mkubwa. Anapewa uraia wa nini huku mchezaji mwenyewe hana hata mwaka mmoja Tanzania? Ni jambo serious na sisi tupo nalo serious,” amesema Magori.

Ameeleza kwamba mashabiki wa Simba wameonesha hasira kubwa kutokana na hali hiyo. “Mashabiki wetu wametaharuki, wanaona yanayotokea, lakini niwasihi watulie. Sisi Simba ni timu inayoweka mpira wa miguu mbele. Najua mpira una hasira kubwa, lakini Bodi tunalishughulikia na tumeiandikia mamlaka. Tutakutana nao na watatuambia kwanini mamabo haya yanatokea mara kwa mara,”.