VITA vya Simba na Yanga haijaishia uwanjani pekee katika kusaka alama tatu bali imehamia hadi katika usajili baada ya vigogo hao kuingia katika upinzani mwingine wa kusaka saini ya mshambuliaji wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Souleymane Fofana.
Fofana ambaye ameonekana kuwa lulu kutokana na kiwango chake bora katika ligi anayocheza kwa sasa na kushawishi mabosi hao wa Kariakoo kutunishiana misuli ya fedha kupata huduma yake.
Taarifa zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo ameanza kuvutia macho ya klabu mbalimbali Afrika, huku Yanga na Simba zikiwa mstari wa mbele kuwania saini yake kwa ajili ya kujiimarisha kuelekea msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Inaelezwa kuwa mawasiliano ya awali tayari yamefanyika kupitia wakala wa mchezaji huyo, ambapo pande zote mbili zimeonyesha nia ya dhati ya kutaka huduma yake, hali inayoweza kusababisha ushindani mkali wa kimaslahi kati ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kwa upande wa Yanga, mabingwa hao wanatajwa kuhitaji kuongeza makali zaidi safu yao ya ushambuliaji ili kuendelea kutawala Ligi Kuu na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa, jambo linalowasukuma kuingia sokoni kwa nguvu.
Nayo Simba haiko nyuma, kwani inaonekana kuweka mipango kabambe ya kurejesha ubora wake kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa, hasa eneo la ushambuliaji ambalo limekuwa likihitaji maboresho ya mara kwa mara.
Licha ya ushindani huo, bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa hadi sasa, huku dau la mchezaji huyo likitajwa kuwa linaweza kupanda kutokana na mvutano wa klabu hizo mbili zinazowania saini yake.
Endapo dili hilo litakamilika, basi linaweza kuwa moja ya usajili mkubwa utakaotikisa soka la Tanzania, huku mashabiki wa Yanga na Simba wakisubiri kwa hamu kuona nani ataibuka mshindi katika mbio hizo.