OFISA Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesisitiza kuwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni mgumu na kwamba kikosi chake hakitakiwi kuteleza wala kuangusha pointi muhimu.
Kamwe aliyasema hayo wakati Yanga ikiendelea na maandalizi ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Pamba Jiji FC, utakaopigwa kesho katika Uwanja wa CCM Kirumba, mkoani Mwanza. Aliongeza kuwa kila alama ni muhimu katika mbio za kushindana kileleni mwa ligi.
“Mungu ametujaalia sahihi tofauti ya alama imerudi kuwa tatu (3). Hatutakiwi kuteleza wala kuangusha alama tena kwa maana ligi ni ngumu. Tunapaswa kupambana na sisi kama Yanga tumeshakubaliana kwamba mzunguko wa pili tusiwe watu wa kulalamika,” amesema Kamwe.
Amesema timu imejipanga kikatili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza mwanzoni mwa msimu hazijarudi tena.
“Sisi ni timu kubwa, tumeshazungumza kuhusu changamoto ambazo zimejitokeza toka mwanzo wa msimu. Wale waliokuwa na wasiwasi wameelewa, na wale ambao walibeza tumeomba wanyamazeni tuendelee na kazi, umuhimu wa umoja ndani ya kikosi cha Yanga,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa kila mchezaji anapaswa kuwa na malengo ya pamoja na kuzingatia nidhamu ili kufanikisha ushindi. Aliongeza kuwa mwakilishi wa timu lazima awe na ari na kujituma kikamilifu katika kila mechi.
Ofisa habari huyo ameeleza kuwa maandalizi ya kiufundi ni muhimu lakini msukumo wa kisaikolojia kwa wachezaji ni sawa na umuhimu wake.
Amesisitiza kuwa kocha na kikosi cha ufundi wanapaswa kuhakikisha wachezaji wanaendelea kuwa na morali ya juu na kuendelea kujiandaa kikamilifu kwa kila mpira wa mechi.
Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani kwa ari kubwa kesho dhidi ya Pamba Jiji FC, wakiwa na lengo la kuhakikisha wanapata matokeo chanya na kuimarisha nafasi yao katika mstari wa juu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kamwe ameongeza kuwa hakuna nafasi ya kulalamika, bali ni kushirikiana na kupigana hadi mwisho wa msimu.