KITENDO cha Simba kutoka sare na Pamba Jiji FC katika mchezo wa hivi karibuni kimeonekana kuwa funzo kwa wapinzani wao Yanga, hasa katika mbinu za kumkabili kiungo hatari wa timu hiyo, Kelvin Nashon.
Katika mchezo huo dhidi ya Simba, Nashon alionyesha kiwango bora na kuwa tishio kubwa uwanjani, huku timu zote zikigawana alama. Hali hiyo imeifanya Yanga kuingia dimbani leo ikiwa na tahadhari maalum dhidi ya nyota huyo.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani jioni hii kuikabili Pamba Jiji FC katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ikiwa na lengo la kuvuna alama tatu muhimu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi kiko katika hali nzuri, kikiwa na ari na morali ya juu ya kuhakikisha kinapata ushindi.
Kamwe amekiri ubora wa wapinzani wao, akieleza kuwa Pamba Jiji ni miongoni mwa timu zinazokuja kwa kasi kwenye soka la Tanzania kwa sasa, hivyo wanahitaji umakini mkubwa.
“Naukubali ubora wa Pamba Jiji, ni moja ya timu bora kwa sasa nchini. Tunatambua walivyocheza dhidi ya wapinzani wetu na kupata alama moja. Hata hivyo, tumejipanga na tumepata mbinu ya kumdhibiti Nashon,” amesema Kamwe.
Amesisitiza kuwa kucheza ugenini si kikwazo kwa Yanga, akibainisha kuwa uzoefu wao wa kushinda mechi za ugenini msimu uliopita uliwasaidia kutwaa ubingwa, hivyo wana imani ya kufanya vizuri tena.