KUELEKEA mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United, safu ya ulinzi ya Simba chini ya Kocha Mkuu, Steven Barker, imezidi kuimarika huku ikipewa msisitizo wa kuepuka makosa yanayoweza kugharimu mabao ya kizembe.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Barker amesema kikosi chake kinapaswa kubaki imara kwa dakika zote 90 ili kuzuia makosa madogo yanayoweza kuwapa wapinzani nafasi ya kufunga.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, kuwavaa wenyeji wao Tabora United katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Kocha huyo ameeleza kuwa maandalizi ya timu yamekuwa mazuri, huku benchi la ufundi likiendelea kuweka mkazo kwenye uimara wa safu ya ulinzi.
Amesisitiza kuwa mechi nyingi huamuliwa katika dakika za mwisho, hivyo ni muhimu kwa wachezaji kuwa makini kwa muda wote wa mchezo.
Barker ameongeza kuwa tangu ajiunge na Simba, timu imeonyesha maendeleo mazuri katika eneo la ulinzi, ingawa bado kuna nafasi ya kuboresha zaidi ili kuifanya timu kuwa ngumu kufungwa na kuwanyima wapinzani nafasi za kutengeneza mashambulizi.
“Siwezi kuzungumzia sana mwanzo wa msimu, lakini tangu nilipokuja hapa nafikiri tumefungwa mabao matatu tu. Hilo ni eneo muhimu sana kwa sababu mechi nyingi huamuliwa katika dakika za mwisho,” amesema Barker.
Amesisitiza kuwa licha ya umuhimu wa kuanza mchezo kwa kasi, jambo la msingi zaidi ni kudumisha umakini, nidhamu na mpangilio mzuri hadi dakika ya mwisho ili kumaliza mechi kwa nguvu.
Awali mchezo huo uliokuwa uchezwe dhidi ya TRA uliahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mkoani Arusha, lakini sasa Simba ipo tayari kurejea dimbani kuendeleza harakati zake za ligi.