KIWANGO bora kinachoonyeshwa na nyota wa Yanga, Allan Okello, kinaendelea kuwasha moto ndani ya kikosi hicho, hali inayomfanya Kocha Mkuu, Pedro Gonçalves, kuanza kutoa tahadhari kwa wapinzani wake.
Yanga leo inatarajiwa kushuka dimbani kuikabili Muembe Makumbi City ya Zanzibar katika michuano ya Kombe la Muungano 2026, huku jina la Okello likiwa gumzo kutokana na ubora wake wa hivi karibuni.
Ubora huo ulidhihirika zaidi kwenye ushindi mkubwa wa mabao 6-0 dhidi ya Mbeya City, ambapo Okello alitoa kiwango cha hali ya juu kilichoacha maswali kwa wapinzani juu ya namna ya kumkabili.
Akizungumzia kiwango cha mchezaji huyo, Kocha Pedro ameweka wazi kuwa si cha bahati mbaya, bali ni matokeo ya jitihada binafsi na nidhamu ya hali ya juu mazoezini na uwanjani.
Mbali na uwezo wake wa kuchezesha timu, Okello anaendelea kung’ara kwenye takwimu, akiwa kinara wa asisti katika Ligi Kuu akiwa na asisti sita, akiwazidi wachezaji wengine kama Duke Abuya na Ellie Mpanzu.
Pedro amesisitiza kuwa Okello ni mchezaji mwenye akili kubwa ya mpira na anayejituma ipasavyo, akionya kuwa huu ni mwanzo tu wa hatari ambayo wapinzani wanapaswa kujiandaa nayo mapema.
Kwa ujumla, kiwango cha Okello kinaendelea kuwa silaha muhimu kwa Yanga, huku mashabiki wakitarajia makubwa zaidi kutoka kwake kadri msimu unavyoendelea.
Katika mchezo wa leo, Yanga watashuka dimbani saa 1:00 usiku kuikabili Muembe Makumbi City FC visiwani Zanzibar, katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani.
Muembe Makumbi City, inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, kwa sasa inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 33 baada ya michezo 22. Licha ya nafasi hiyo, timu hiyo haiwezi kubezwa kwani mara nyingi huongeza ari wanapokutana na vigogo.
Kwa upande wa Yanga, wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 47 katika michezo 22. Kikosi hicho kinaonekana kuwa imara zaidi msimu huu, kikijivunia safu kali ya ushambuliaji iliyofunga mabao 44 huku ulinzi wake ukiruhusu mabao matatu pekee.