DIWANI wa Kata ya Kariakoo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Haji Manara ametoa kauli yenye kujirudia ambayo tafsiri yake ya moja kwa moja ni usaliti dhidi ya mpira.
Manara ambaye kwa asilimia kubwa umarufu wake umetokana na mpira, amekuwa akitoa kauli zenye kuumiza hisia za watu wa mpira kuhusu uwanja mkongwe zaidi hapa nchini, Kumbukumbu ya Karume.
Mapema mwezi Machi, Manara alijirekodi video moja akitoa hoja ya serikali ya Jiji la Dar es Salaam kuupora Uwanja wa Karume. Alisema uwanja huo ulikuwa mali ya Jiji la Dar es Salaam, ukatolewa kwa FAT kwa ajili ya michezo, lakini haujaendelezwa hadi sasa.
Kwa hiyo serikali ya jiji iuchukue na kubadilisha matumizi, kwa kujenga maegesho ya magari.
Akairudia tena kauli hii mapema Aprili, akiwa kwenye kipindi cha redio moja hapa nchini, ambayo anafanyia kazi kwa sasa. Ukimsikiliza kwa makini na kuusoma uso wake wakati anaongea, anaonekana kabisa ni mtu aliyedhamiria kufanya anachokisema.
Yaani Manara amedhamiria kuudhulumu mpira kwa kupora uwanja wa Karume ili eneo lile ligeuzwe maegesho ya magari.
Huyu ni Manara, mtu aliyezaliwa na kulelewa kwenye mpira, na akaishi kwenye mpira na kuupata umaarufu wote anaoringa nao sasa. Malalamiko ya watu wa mpira kwa miaka yote ni mchezo huu pendwa unakosa watu wa kuutetea kwenye ngazi za maamuzi.
Watu kama kina Manara wanaposhika nafasi muhimu za maamuzi, matarajio ni wataupigania mpira…lakini badala yake wanaupiga vita.
Kwa kauli zake hizi kuhusu Uwanja wa Karume, Manara ametangaza vita kubwa sana na mpira.
Ameshika silaha nzito kupigana na mpira na hii haiwezi kuachwa hivi hivi. Anaingia kwenye vikao vya Halmashauri ya Jiji kama diwani.
Lakini zaidi, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mipango Miji na Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Na tusisahau ni mzuri sana kwenye kuongea na kujenga hoja.
Akitumia kipawa hiki katika vikao vya Halmashauri ya Jiji, maana yake Uwanja wa Karume unaweza kuchukuliwa. Hapo ndipo kwenye zingatio kuu la andiko hili.
Familia ya mpira inatakiwa kuanza kupiga kelele kuanzia sasa kupinga matamanio haya ya Manara.
Moja ya tetesi za sababu ya Manara kuukomalia Uwanja wa Karume ni kinachodaiwa ni tofauti zake na Wallace Karia.
Manara alifungiwa kwa muda mrefu na TFF baada ya kukwaruzana na Karia kama Rais wa TFF, mwaka 2022 kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, jijini Arusha.
Kuanzia hapo Manara na Karia wakawa hawapikiki chungu kimoja na sasa Manara ana madaraka, analipa kisasi.
Hii ni tetesi, lakini kama ni kweli, Manara atakuwa anaukosea zaidi mpira. Ugomvi binafsi hauwezi kuidhuru familia nzima ya mpira…si sawa.
KUHUSU UWANJA WA KARUME
Manara anadai uwanja huu ulikuwa Mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na ikaugawa kwa mamlaka za mpira ili kusaidia maendeleo ya mchezo huo. Hii ni taarifa mpya sana, tofauti na kumbukumbu nyingi za zamani. Maandiko mengi yanautaja Karume ulikuwa mali ya shirika la reli na pale palikuwa railway club, yaani kituo cha starehe cha shirika la reli.
Wakati huo (miaka ya 1920 na kuendelea), uwanja mkuu wa mpira ulikuwa pale Mnazi Mmoja ambapo sasa kuna uwanja wa mikutano.
Baadaye serikali (ya mkoloni), ikahamisha uwanja wa michezo (mpira) kutoka Mnazi Mmoja hadi uwanja wa Railway, na ndipo jina likabadilika kutoka Railway club hadi Ilala Stadium.
Yakaanzishwa mashindano ya mpira na bingwa alipaswa kupewa ule uwanja wa Mnazi Mmoja.
Klabu ya Sunderland ikashinda ubingwa lakini serikali ikabadili mawazo, uwanja ule ukawa wa mikutano.
Wakati huo uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ulikuwa Kurasini, katika eneo ambalo sasa kuna uwanja wa taifa, chuo kikuu cha DUCE, shule ya Jitegemee hadi jeshi la wokovu.
Mwaka 1954 uwanja wa ndege ukahama kutoka eneo lile hadi Kipawa. Lile eneo likagawanywa kwa matumizi tofauti, kipande kimoja kikawa uwanja wa michezo…ndipo ukajengwa uwanja wa taifa…sasa uhuru na Mkapa.
Kwa hiyo uwanja mkuu wa michezo ukawa pale na uwanja wa Ilala ukakabidhiwa kwa chama cha mpira TFA (Tanganyika Football Association), hii ni kabla ya kuanza kwa FAT na baadaye TFF.
Ni kwamba eneo lile lilikuwa la michezo tangu mwanzo…na lilianza kumilikiwa na shirika la reli, baadaye serikali.
Sasa hiyo serikali kama ilikuwa ya mji wa Dar es Salaam au serikali kuu, sio jambo la muhimu…kilicho muhimu ni eneo lile lilikuwa la michezo tangu mwanzo.
Manara anapotaka kutumia nafasi yake kulipora na kuligeuza maegesho, sio sawa hata kidogo.
Uwanja ule ndio aliocheza baba yake mzazi, Sunday Manara, na kupata sifa zote alizopata hadi kuitwa Computer.
Leo anapotaka kufanya anachofanya ni usaliti mkubwa na unatakiwa kukemewa vibaya.