Home Habari za michezo VIWANGO VYA UBORA CAF…SIMBA ZIIII…KUTOKA NO 5 MPAKA 11….YANGA MHHHH…..

VIWANGO VYA UBORA CAF…SIMBA ZIIII…KUTOKA NO 5 MPAKA 11….YANGA MHHHH…..

0
Habari za Michezo leo

BAADA ya Simba kuwa na msimu mgumu katika michuano ya kimataifa 2025-2026, imejikuta ikiporomoka kwenye orodha ya viwango vya ubora vya klabu iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Orodha hiyo mpya imetolewa baada ya kukamilika kwa mechi za nusu fainali za michuano ya CAF na ilishuhudiwa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na AS FAR Rabat ya Morocco zikitinga fainali ya Ligi ya Mabingwa, huku USM Alger (Algeria) na Zamalek (Misri) nazo zikitinga fainali upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba ambayo msimu huu Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi iliburuza mkia kundi D na pointi tano nyuma ya Stade Malien, Esperance de Tunis na Petro de Luanda, imeshika nafasi ya 11 katika orodha hiyo inayoongozwa na Mamelodi Sundowns kwa mujibu takwimu za miaka mitano ya ushiriki wa mashindano ya CAF.

Yanga imeendelea kusogea nafasi za juu kwenye orodha hiyo baada ya kuwa nafasi ya 12 huku wakizizidi kete, Wydad Casablanca ya Morocco, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na TP Mazembe ya DR Congo.

Azam yenyewe taratibu inajikongoja kufuatia msimu huu kuweka rekodi kwa kucheza hatua ya makundi na kuwa timu pekee ya Tanzania iliyokusanya pointi nyingi zaidi (tisa) katika hatua hiyo, ipo nafasi ya 38 sawa na Singida Black Stars.

Simba misimu hiyo mitano ukiwemo huu, imefika robo fainali kimataifa mara tatu na msimu wa 2021-22 ilikuwa Kombe la Shirikisho, 2022-23 na 2023-24 ikiwa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu uliopita Simba ikiwa chini ya kocha Fadlu Davids ambaye kwa sasa anaifundisha Raja Casablanca ya Morocco, ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-1, katika mechi ya kwanza ilipoteza kwa mabao 2-0 huku ikitoa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Simba imeshika nafasi hiyo ikiwa na pointi 38 ambazo zimetokana na mafanikio ambayo wameyapata ndani ya misimu hiyo, Yanga yenye pointi 35, imeshika nafasi hiyo ikifika robo fainali mara moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-24 huku ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-23.

Yanga ikiwa chini ya Nasreddine Nabi, ilibaki kidogo ibebe ubingwa wa Afrika msimu huo mbele ya USM Alger lakini iliangushwa na kanuni ya bao la ugenini, ilipoteza fainali ya kwanza nyumbani kwa mabao 2-1 wakati ikiwa ugenini ikaibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika misimu miwili ya mwisho, 2024-25 na 2025-26, Yanga imeishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku msimu wa 2021-22 ikiishia raundi ya kwanza na ilitolewa na Rivers United kwa jumla ya mabao 2-0.

Azam imesogea hadi nafasi hiyo kutokana na mafanikio yao ya msimu huu, ikiwa chini ya Florent Ibenge, kufika kwao hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi B nyuma ya Wydad na AS Maniema Union kumewafanya kufikisha pointi tano.

Singida Black Stars ni kama Azam, iliishia makundi Kombe la Shirikisho na kukusanya pointi tano.

MWAKA 2025

Kwa mujibu wa viwango vya ubora wa mwaka jana 2025 ambavyo vilitolewa na CAF, Simba ikuwa nafasi ya tano ikiwa na pointi 48, hivyo imeshuka kwa nafasi tano, mabadiliko mengine katika nafasi hizo za juu ni katika nafasi ya kwanza na pili na mwaka jana, orodha hiyo iliongozwa na Al Ahly huku Mamelod ikiwa nafasi ya pili.

Wengine ambao walikuwa juu ya Simba katika nafasi ya tatu na nne, walikuwa ni Espérance Sportive de Tunis na RS Berkane ambao wameendelea kukomaa nafasi hizo, awamu hii Mnayama amezidiwa kete na Zamalek (Misri), Pyramids (Misri), USM Alger (Algeria), AS FAR (Morocco) na Al Hilal (Sudan).

Yanga imeendelea kushikilia nafasi ya 12 huku Namungo ikiwa nafasi ya 75 ikiwa na pointi 0.5, wakati huo, Azam haikuwa katika orodha hiyo.