Tukiangalia kwa upana zaidi, West Ham wamekusanya pointi 19 katika mechi 12 zilizopita, Forest wana pointi 18 katika mechi 13 na Leeds pia wana pointi 18 lakini katika mechi 14. Tangu waifunge Crystal Palace Desemba 28, Spurs wamekusanya pointi sita katika mechi 15.
MECHI ZILIZOSALIA
Kila mwaka ratiba inapotangazwa hakuna shaka kwamba muda wa kukutana na timu fulani unaweza kuwa na athari kubwa katika kipindi chote cha msimu wa miezi 10.
Zikiwa zimesalia mechi tano, Spurs wataamini kwamba ratiba iliyobaki angalau kwenye makaratasi inawapa nafasi kubwa ya kubaki ligi kuu. Mechi inayofuata ni ugenini dhidi ya Wolves, ambao tayari wameshuka daraja.
Pia watakuwa na mechi ya nyumbani dhidi ya Leeds Mei 11, ambayo wataiona kama fursa nyingine nzuri, hasa kama Leeds watakuwa tayari wamejihakikishia usalama wao kwa kuifunga Burnley katika mechi yao iliyotangulia.
Hata mechi ngumu ugenini dhidi ya Aston Villa Mei 3 inakuja wakati mzuri kwa Spurs, kwani itachezwa katikati ya michezo miwili ya nusu fainali ya Europa League kwa timu hiyo.
Watakwenda kwa wapinzani wao Chelsea kabla ya kuikaribisha Everton katika siku ya mwisho ya msimu siyo mechi rahisi hizo, hasa kwa kuwa timu zote mbili zinaonekana kupigania nafasi ya michuano ya Ulaya. Lakini kutokana na ushindani ulivyo mkali, hilo ni jambo ambalo timu zote zinazopambana kuepuka kushuka daraja zitalazimika kukabiliana nalo. West Ham wataikaribisha Everton Jumamosi kabla ya kusafiri kwenda kucheza na Brentford na ratiba yao itakuwa ngumu zaidi watakapocheza na Arsenal Mei 10.
Hata kama Newcastle United imekuwa maji kupwa na maji kujaa, kucheza ugenini katika Uwanja wa St James Park siyo kazi rahisi na mechi yao ya mwisho nyumbani dhidi ya Leeds inaweza kuwa na umuhimu mkubwa.
Kwa upande wa Forest, wao wana ratiba ngumu zaidi, wakiwa na mechi za ugenini dhidi ya Chelsea na Manchester United mwezi Mei.
Mechi za nyumbani dhidi ya Newcastle na Bournemouth siku ya mwisho zinaweza kuwa muhimu sana, lakini kupata matokeo dhidi ya Sunderland Ijumaa kutasaidia kupunguza presha kabla ya kumaliza msimu.