KOCHA Mkuu mpya wa Mbeya City, Salum Mayanga, ameweka wazi mkakati wake wa kuisuka upya timu hiyo ili kuhakikisha inasalia salama katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Mayanga amechukua nafasi ya Mecky Maxime aliyeondoka ndani ya klabu hiyo kufuatia kipigo kizito cha mabao 6-0 kutoka kwa Yanga, matokeo yaliyotikisa kikosi hicho na kuhitaji mabadiliko ya haraka ya kiufundi.
Akizungumza kuhusu majukumu yake mapya, Mayanga amesema hatakuja na mbinu za kimiujiza bali ataendeleza juhudi zilizoanza na waliomtangulia, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kukusanya pointi muhimu katika michezo iliyosalia.
Ameeleza kuwa, licha ya changamoto zilizopo, ana imani na msingi uliowekwa na benchi la ufundi lililopita, hasa katika uwezo wa timu kupata matokeo chanya katika baadhi ya mechi walizocheza.
“Kurudi kwangu siyo kwamba nitaleta miujiza ya haraka kuifanya timu ibaki salama. Ukweli ni kwamba kuna kazi kubwa mbele yetu, na inahitaji kujitoa kwa kiwango cha juu kutoka kwa kila mmoja,” amesema Mayanga.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya timu hiyo yatategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya uongozi, benchi la ufundi na wachezaji, huku nidhamu na kujituma vikipewa kipaumbele kuanzia mazoezini hadi siku za mechi.
Mayanga ameongeza kuwa anatambua ukubwa wa jukumu alilonalo, lakini yuko tayari kuendeleza pale walipoishia waliomtangulia ili kuhakikisha Mbeya City inavuka salama na kubaki kwenye ushindani wa ligi hiyo.