KIUNGO wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amesema kikosi chao kipo tayari kwa vita ya kusaka tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Muungano, wakifahamu wazi kuwa wanakwenda kukutana na mpinzani mwenye hadhi kubwa na ushindani wa hali ya juu.
Azam FC wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, ambapo sasa wanatarajiwa kukutana na Yanga katika mchezo utakaopigwa Jumamosi, Aprili 25, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Fei Toto ameweka wazi kuwa malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanapambana kwa nguvu zote katika kila mechi ili kupata matokeo chanya yatakayowawezesha kusonga mbele zaidi.
Amesisitiza kuwa ndani ya kikosi hicho kuna morali ya hali ya juu, huku wachezaji wakiwa tayari kukabiliana na changamoto yoyote watakayokutana nayo uwanjani, bila kujali ukubwa wa mpinzani.
“Tunatambua tunakutana na Yanga, ni timu kubwa, lakini na sisi ni timu kubwa. Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunapambana na kutwaa taji la Kombe la Muungano,” amesema Fei Toto.
Kungo huyo ameongeza kuwa maandalizi ya kila timu ni jambo la msingi katika kufanikisha malengo, akibainisha kuwa wakati Yanga wakiendelea na programu yao, Azam FC nao hawako nyuma katika kuhakikisha wanakuwa kwenye kiwango bora.
Kwa kauli hiyo, ni wazi kuwa pambano hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku kila timu ikiingia uwanjani ikiwa na dhamira ya kuibuka na ushindi na kusonga hatua ya fainali.