Habari za michezo

BARCA YAACHANA NA RASHFORD, SANCHO AKITEMWA MAN UNITED

Vardo June 10, 2026 3:45 pm

BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA imeripotiwa kusitisha mpango wa kumsajili Marcus Rashford na sasa mshambuliaji huyo wa England atarejea Manchester United baada ya kukataa kulipa ada ya takriban Pauni 26 milioni iliyokuwa sehemu ya makubaliano ya mkopo.

Rashford, 28, ambaye yupo chini ya mkataba wa Manchester United, alikuwa amepewa nafasi ya kujiunga rasmi na Barcelona, lakini klabu hiyo  haipo tayari kulipa kiasi hicho cha fedha na ripoti zinaeleza kuwa Barca walipendekeza kulipa nusu ya bei hiyo (Pauni 13 milioni), lakini United walikataa ofa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Barcelona wameamua kuendelea na wachezaji wengine wa safu ya ushambuliaji akiwemo Anthony Gordon ambaye wanadaiwa kumsajili kutoka Newcastle United kwa takriban Pauni 70 milioni na sababu iliyotajwa ni pamoja na uwezo wake wa kujilinda, ambayo inasemekana ni sehemu dhaifu kwa Rashford, pamoja na tofauti ya umri.

Barcelona pia wanaripotiwa kuangalia chaguo jingine kama Bernardo Silva kwa uhamisho wa bure na Julian Alvarez kama mbadala wa Robert Lewandowski. Wakati huohuo, Rashford anahusishwa na klabu kadhaa ikiwemo Arsenal, Tottenham Hotspur na Aston Villa, ambayo alicheza kwa mkopo msimu uliopita.

Klabu nyingine kubwa kama Real Madrid na Bayern Munich pia zimetajwa kuwa na uwezekano wa kumtaka. Hata hivyo, mshahara wake mkubwa wa takriban Pauni 315,000 kwa wiki pamoja na umri wake (atakayefikisha miaka 29 Oktoba) vinaonekana kuwa changamoto kwa timu nyingi. Inaaminika huenda akalazimika kukubali kupunguza mshahara au kuvunja mkataba ili kupata uhamisho wa kudumu. Iwapo suluhu haitapatikana kabla ya maandalizi ya msimu (pre-season), Rashford anaweza kurejea Carrington, hali ambayo inaweza kumuweka tena katika kundi la wachezaji ambao United walikuwa tayari kuwauza au kuwakotoa kwa mkopo.

Hali kama hiyo pia inamhusu kipa Andre Onana ambaye baada ya mkopo Trabzonspor ameripotiwa kukosa nafasi ya muda mrefu Old Trafford, huku klabu ikitafuta suluhu ya kumuuza au kumtoa kwa mkopo mwingine.

Katika hatua nyingine, Jadon Sancho aondoka Manchester United bila ada baada klabu hiyo kuthibitisha kuwa winga hayupo katika mipango yake, akidumu miaka mitano tangu aliposajiliwa kwa Pauni 73 milioni.

Sancho, ambaye alikuwa akilipwa takriban Pauni 250,000 kwa wiki, anahitimisha kipindi chake Old Trafford akiwa amecheza mechi 83 kwa klabu hiyo na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda Carabao 2023, lakini baadaye alitumia muda wake kwa mikopo katika klabu tofauti zikiwemo Borussia Dortmund, Chelsea na Aston Villa.

Katika taarifa fupi, Manchester United pia imesema inaachana na Casemiro pamoja na Tyrell Malacia. Uamuzi huo unaashiria mabadiliko makubwa ya kikosi ambacho kinaendelea kujipanga upya baada ya misimu ya matokeo yasiyo thabiti.

ENGLAND YATUMIA WAKE, WAPENZI KUWAPA WACHEZAJI UTULIVU MAREKANI