Chasambi Afichua Sababu za Kutua Singida BS, Aingia Vita ya CECAFA Kagame
Kiungo mpya wa Singida Black Stars, Ladack Chasambi, amefunguka kuhusu sababu zilizomfanya achague kujiunga na miamba hiyo ya Singida, akitaja fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa kama nguzo kuu ya maamuzi yake.
Chasambi, ambaye amejiunga na Singida BS akitokea Simba SC, ameeza kuwa mradi kabambe wa klabu hiyo pamoja na malengo yake ya kurejea kwenye anga za kimataifa viliivutia nafsi yake ili kupata jukwaa la kuonyesha kiwango cha juu.
Baada ya kupitia kipindi cha uchache wa nafasi ya kucheza akiwa na Wekundu wa Msimbazi, kiungo huyo anaamini kuwa Singida Black Stars ni sehemu sahihi ya kufufua na kuendeleza kipaji chake.
⚽ Kupambania Kombe la Shirikisho na CECAFA
Singida Black Stars inajiandaa kuwakilisha nchi kwa mara ya pili mfululizo katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC). Hivi sasa kikosi hicho kipo nchini Rwanda kikishiriki Kombe la CECAFA Kagame kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya.
“Moja ya vitu vilivyonivutia kuja Singida ni kuona timu ina malengo makubwa, hasa kushiriki mashindano ya kimataifa. Hii ni nafasi nzuri kwangu kama mchezaji kujipima na kusaidia timu kufikia malengo yake,” alisema Chasambi.
💥 Ushindani na Kutetea Taji
Akizungumzia ushindani wa namba na ratiba inayowakabili, Chasambi amekiri kuwa kibarua kitakuwa kizito lakini maandalizi mazuri na mshikamano kikosini ndio zitakuwa nguzo kuu za mafanikio.
“Kikosi kina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa na viongozi wana maono mapana. Wajibu wetu ni kufanya mazoezi kwa bidii, kufuata maelekezo ya mwalimu na kujenga timu yenye ushindani,” aliongeza.
Pia, kiungo huyo ameweka wazi hamu yake ya kutwaa taji la CECAFA Kagame akiwa na Singida BS na kusaidia timu hiyo kutetea heshima yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.