Katwila: Geita Gold Kumva Yanga Ki-Timu, Sio Mchezaji Mmoja Mmoja
KOCHA Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kukabiliana na kibarua kizito dhidi ya Yanga SC kesho katika mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akisisitiza kuwa siri ya ushindi wao itakuwa ni mchezo wa ki-timu badala ya kutegemea uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Geita Gold inaingia katika mchezo huo ikitambua ugumu uliopo mbele yao, huku Katwila akikiri kuwa ubora na ukubwa wa Yanga unawalazimisha kufanya maandalizi ya kiwango cha juu ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Maandalizi ya Ki-Timu na Nidhamu Katwila ameeleza kuwa maandalizi yao yamejikita katika kuwajenga wachezaji kucheza kwa ushirikiano na nidhamu ya hali ya juu ili kuhimili mikimiki ya wapinzani wao.
“Level ya mpinzani ni kubwa kwa sababu ni mchezo mwingine mkubwa kwetu. Lazima ujiandae vizuri kucheza na mpinzani ambaye level yake ni kubwa,” amesema Katwila.
Kocha huyo aliongeza kuwa nidhamu ya kitimu ndiyo nguzo kuu itakayowapa nafasi ya kushindana vyema uwanjani:
“Tunajiandaa kucheza ki-timu zaidi. Huwezi kucheza kwa mchezaji mmoja mmoja. Lazima tucheze ki-timu ili kuweza kukabiliana na Yanga, ambayo ni timu bora.”
Heshima kwa Wapinzani, Hakuna Dhana ya Uchovu Kuhusu uwezekano wa Yanga kuwa na uchovu kutokana na ratiba ngumu ya michezo ya kimataifa, Katwila amepuuza dhana hiyo na kusisitiza kuwa maandalizi yake hayajajengwa kwenye nadharia za kufikirika, bali katika kukabiliana na Yanga ikiwa kwenye ubora wake wa juu.
“Kusema kuna uchovu ni maana naanza kujidanganya kwamba wao ni wachovu. Hapana. Lazima umpe ubora wake na ukubwa wake ili uweze kujiandaa vizuri zaidi,” amesisitiza.
Saikolojia na Kutumia Makosa ya Yanga Pia amebainisha umuhimu wa kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia kabla ya kuingia uwanjani, kwani Yanga itaingia ikiwa na kujiamini kikubwa kutokana na uzoefu wa mechi za kimataifa.
“Psychology ya wachezaji wangu lazima iwaandae kucheza na timu bora. Wataenda wakiwa na hisia kwamba wanacheza na timu bora ambayo imetoka kucheza mchezo wa kimataifa na ina confidence nzuri.”
Hata hivyo, Katwila amebainisha kuwa wataingia kwa umakini bila kulazimisha mambo, wakisubiri fursa zitakazotokana na makosa ya wapinzani wao ili kuadhibu.
“Kwa sisi tutakachoangalia ni jinsi gani watakavyofanya makosa. Kama watakuwa makini, basi sisi ndio tunaweza kutumia hizo nafasi.”
Akimalizia, Katwila ameeleza kufurahishwa na fursa ya kukutana na timu kubwa kama Yanga, kwani mechi za aina hii huwapa wachezaji wake kipimo sahihi cha uwezo wao na uzoefu wa kushindana katika kiwango cha juu.