Djibouti U-20 Yawasili Tanzania Kuwania Tiketi ya AFCON CECAFA
TIMU ya taifa ya Djibouti ya vijana chini ya miaka 20 imewasili nchini Tanzania ikiwa na lengo moja kuu: kupambana hadi kufikia fainali za michuano ya CECAFA U-20 ili kujakatia tiketi ya kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-20) mwaka 2027 nchini Ghana.
Kikosi hicho kilitua nchini juzi Jumamosi tayari kwa kinyang’anyiro hicho kinachotarajiwa kutimua vumbi kuanzia Septemba 15 hadi 25, 2026.
Maagizo na Hamasa Kutoka kwa Viongozi Kabla ya kuanza safari yao, wachezaji wa Djibouti waliagwa kwa hafla maalum iliyofanyika katika kituo chao cha akademi ya soka. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka la Djibouti pamoja na viongozi waandamizi, akiwemo Mkurugenzi wa Shirikisho, Hassan Ali, na Mkuu wa Msafara, Said Bouha.
Viongozi hao waliwasisitizia vijana hao umuhimu wa kucheza kwa nidhamu, kujituma, na kuiwakilisha nchi yao kwa heshima kubwa katika kila mechi.
Kundi B: Mtihani Mzito Dhidi ya Uganda na Sudan Djibouti imepangwa katika Kundi B pamoja na timu ngumu za Uganda na Sudan. Viongozi wamewatahadharisha wachezaji kuwa kila mchezo utakuwa kama fainali, kwani makosa madogo katika mechi za mwanzo yanaweza kuwagharimu na kuondoa ndoto zao za kusonga mbele.
Ili kufuzu Fainali za AFCON U-20 mwaka 2027, Djibouti inatakiwa kufika hadi hatua ya fainali ya michuano hii ya CECAFA, kwani ni timu mbili pekee zitakazocheza fainali ndizo zitakazowakilisha ukanda wa CECAFA.