Carroll Aichana England: “Rooney Alikuwa Akivuta Sigara na Kunywa Bia Kambini”
LONDON, ENGLAND — MAMBO mazito yameibuka ndani ya kikosi cha zamani cha Timu ya Taifa ya England (Three Lions), baada ya mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Andy Carroll, kufichua siri za ndani za kambi akimnyoshea kidole staa mwenzake Wayne Rooney.
Carroll ameyafichua hayo kupitia kitabu chake kipya cha kumbukumbu za maisha ya soka kinachokwenda kwa jina la “Owning It”, akieleza kwa kina jinsi wachezaji walivyokuwa wakijiburudisha kambini chini ya utawala wa kocha raia wa Italia, Fabio Capello.
“Rooney Alivuta Sigara na Kunywa Bia Room”
Kwa mujibu wa Carroll, Rooney alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakitafuta mbinu za kupunguza msongo wa mawazo na uchovu wa maisha ya kambini.
Carroll anasema Rooney alikuwa akimpigia simu mchana na kumwambia: “Andy, njoo chumbani kwangu sasa.”
Anadai kila alipofika chumbani kwa Rooney, alimkuta mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United akiwa amelala kitandani akitazama runinga huku akivuta sigara na kunywa bia.
Carroll ameongeza kuwa chumba cha Rooney kilikuwa na katoni za sigara, kreti za bia, na chupa za mvinyo zilizowekwa na meneja wa hoteli kwa agizo la Rooney mwenyewe. Hata hivyo, alisisitiza kuwa wachezaji hawakuwa wakilewa kupita kiasi cha kushindwa kuwajibika.
Wayne Rooney Akanusha Vikali Madai Hayo
Mfungaji huyo wa zamani wa mabao 53 katika mechi 120 alizochezea England, Wayne Rooney, ameibuka na kupinga vikali simulizi hiyo akiita kuwa ni uzushi mtupu.
Rooney, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka kwenye runinga, alisema:
“Andy anajua fika kwamba mimi na yeye hatukuwahi kuwa marafiki wa karibu au kushirikiana sana kijamii. Tulikutana kwa bahati mara moja tukiwa likizo, lakini ilikuwa hivyo tu. Kuhusu hii hadithi kwamba nilikuwa nikinywa nikiwa kwenye majukumu ya England, ni uzushi kabisa na inakatisha tamaa sana.”
Utani wa Rooney na Mtaalamu wa Tiba (Physio)
Mbali na tuhuma za pombe na sigara, Carroll amesimulia tukio jingine la utani ambapo Rooney alimfanyia mtaalamu wa tiba ya viungo wa England, Rod Thornley.
Baada ya kuchezewa mchezo wa utani wa kuwabeba wachezaji watatu, Rooney alisisimka na kumrukia Thornley aliyekuwa amelala kwenye meza ya matibabu. Carroll anasema yeye na Steven Gerrard walibaki wakicheka kwa furaha wakati Thornley akipiga kelele chini ya uzito wa Rooney.
“Golden Generation” Ilikuwa na Makundi na Mipasuko
Carroll pia amefichua kuwa kizazi cha dhahabu cha England (Golden Generation)—kilichokuwa na nyota kama Rooney, Steven Gerrard, Frank Lampard, John Terry, Ashley Cole, na Jamie Carragher—kiliingia dosari kutokana na makundi ya kanda.
Anasema kulikuwa na mgawanyiko mkubwa kati ya wachezaji kutoka Kaskazini mwa England na wale wa Kusini:
-
Wachezaji wa klabu za Kaskazini walikaa upande wao, na wa Kusini upande wao.
-
Hali hiyo ilipelekea baadhi ya wachezaji kutozungumza kabisa au hata kusita kupeana pasi mazoezini.
-
Carroll anakiri kuwa yeye alilazimika kujiunga na kundi la Kaskazini.
Nidhamu ya Capello: Simu Zakatzwa, Ketchup Yapigwa Marufuku!
Kuhusu kocha Fabio Capello, Carroll ameeleza jinsi Mwaitaliano huyo alivyokuwa na sheria kali za nidhamu:
-
Suala la Simu: Siku moja Carroll na Ashley Young walipowasili kikaoni dakika 15 kabla ya muda, Capello alimkuta Carroll akitumia simu. Alimnyang’anya kwa hasira na kumtupia kifuani akidai ni dharau.
-
Mvinyo na Ketchup: Capello aliwaruhusu wachezaji kunywa glasi moja ya mvinyo na kula dessert kama keki ya chokoleti na ice cream wakati wa chakula, lakini alipiga marufuku matumizi ya Ketchup (mchuzi wa nyanya).
Carroll amewahi kuhoji: “Haikuwa na maana kabisa kwanini mvinyo na dessert viruhusiwe lakini ketchup ikatwe?”