MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, ameibuka na takwimu nzito zinazoonyesha uimara wa timu hiyo baada ya kukamilika kwa michezo mitano ya mwanzo ya tathmini ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kamwe ameweka wazi namna kikosi hicho kilivyoanza kwa kasi, kikionyesha uthabiti mkubwa uwanjani katika michezo yao mitano ya ligi, huku pia kikiendelea kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Muungano.
Ameeleza kuwa Yanga imefanikiwa kushinda michezo yote mitano iliyocheza, hatua inayoonyesha ubora wa kikosi hicho katika ushindani wa ligi. Mbali na ushindi huo, timu imefunga jumla ya mabao 17, ikiashiria makali ya safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa tishio kwa wapinzani wao.
“Si hilo tu, lakini pia Yanga haijaruhusu bao lolote katika michezo hiyo mitano, jambo linalothibitisha uimara wa safu ya ulinzi pamoja na ubora wa kipa wa timu hiyo. Takwimu hizi zinaipa Yanga hadhi ya kuwa miongoni mwa timu zilizoanza ligi kwa kiwango cha juu kabisa,” amesema Kamwe.
Kamwe amesisitiza kuwa huu ndio ubora wa Yanga, akitumia kauli inayosisitiza msimamo wa timu hiyo: “Hatusemi, hatuchekeshi, tunafanya kweli,” akimaanisha mafanikio hayo si maneno bali ni vitendo vinavyoonekana uwanjani.
Vilevile, amewataka wapinzani wao kukutana nao uwanjani kwa ushindani wa haki, huku akiwataka wachambuzi na wadau wa soka kutumia majukwaa yao kwa uwajibikaji.
Katika hatua nyingine, kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi, Yanga ilifanya tathmini na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Pedro Goncalves, na kufikia uamuzi wa kumuongezea kocha msaidizi Abdulhamid Moalin.
Tangu ujio wa Moalin, Yanga imefanikiwa kucheza mechi tano za Ligi Kuu na kushinda zote, ikiendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi.