MCHEZO wa Kariakoo Derby kati ya Simba SC na Yanga SC unaotarajiwa kuchezwa Mei 3, 2026, katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, unaendelea kuvuta hisia za mashabiki huku taarifa zikieleza kuwa waamuzi wa pambano hilo huenda wakatoka nje ya nchi, kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Safari hii, macho na masikio ya wadau wengi wa soka yameelekezwa kwa “mapirato” wa mchezo huo, ambapo inadaiwa kuwa waamuzi kutoka Morocco watapewa jukumu la kusimamia pambano hilo kubwa la watani wa jadi.
Uamuzi huo unatajwa kuongeza uzito wa dabi hiyo, huku ukitarajiwa kuleta ushindani wa haki na kupunguza malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika michezo ya aina hii yenye presha kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, mwamuzi wa kati atakuwa Hamza El Faruq, akisaidiwa na wasaidizi wake Lahsene Azkawi na Hamza El Nasri, huku Mostafa Kchaaf akiteuliwa kuwa mwamuzi wa akiba (Fourth Official).
Kikosi hicho cha waamuzi kinatajwa kuwa na uzoefu mkubwa katika kusimamia mechi za kimataifa zenye ushindani mkali, jambo linaloongeza imani kwa mashabiki na wadau wa soka kuwa mchezo huo utaendeshwa kwa viwango vya juu.
Hatua ya kuleta waamuzi kutoka nje inaonekana kuwa mkakati mahsusi wa kuhakikisha uwazi na haki vinatawala, hasa ikizingatiwa historia ya Derby ya Kariakoo ambayo mara nyingi imekuwa ikigubikwa na mvutano na hisia kali kutoka kwa pande zote mbili.
Ikumbukwe kuwa msimu uliopita, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Derby ya Kariakoo, uliochezwa Juni 25, 2025, waamuzi walitoka Misri wakiongozwa na Mohamed Amin Omar, hatua iliyosaidia kupunguza malalamiko na kuongeza uaminifu kwa waamuzi.