Home Habari za michezo KWANINI VALVERDE, TCHOUAMENI WALIZICHAPA

KWANINI VALVERDE, TCHOUAMENI WALIZICHAPA

0

MADRID, HISPANIA: NINI kinaendelea kwenye chumba cha wachezaji wa Real Madrid? Msimu wa Real Madrid umeendelea kuwa mbaya zaidi wiki hii baada ya taarifa za migogoro mipya ndani ya kikosi hicho, ikiwemo tukio lililompeleka Federico Valverde hospitalini kutokana na kuumia kichwani baada ya mabishano makali na Aurelien Tchouameni mazoezini.

Mvutano umekuwa mkubwa ndani ya Real Madrid msimu mzima, huku timu hiyo ikielekea kumaliza mwaka wa pili mfululizo bila taji kubwa. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwishoni mwa wiki hii endapo Barcelona watapata sare au ushindi katika El Clasico ya kesho, Jumapili, na kutangazwa rasmi mabingwa wa La Liga.

Ndani ya Real Madrid, hasira kuhusu hali ya timu zimefikia kiwango cha juu, huku chumba cha wachezaji kikielezwa kuwa karibu kugawanyika kabisa.

Jumatano iliripotiwa kuwa kulikuwa na ugomvi mkali mazoezini kati ya Valverde na Tchouameni. Hali ilizidi kuwa mbaya Alhamisi baada ya wawili hao kuripotiwa kugombana tena wakati wa mazoezi mengine, huku tukio hilo likiishia kwa Valverde kupelekwa hospitali.

Valverde aliandika kwenye mitandao ya kijamii kueleza kilichotokea akisisitiza kuwa hakukuwa na kipigo kati yao na kwamba wakati wa mabishano “aligonga meza kwa bahati mbaya,” jambo lililosababisha jeraha kwenye paji la uso lililomlazimu kwenda hospitali kwa uchunguzi.

Real Madrid ilitoa taarifa ikieleza kuwa Valverde alipata majeraha ya kichwani yatakayomuweka nje kwa siku 10 hadi 14. Hivyo ataikosa El Clasico dhidi ya Barcelona katika Uwanja wa Camp Nou, mchezo ambao Real Madrid lazima ishinde ili kubaki na matumaini ya kutwaa La Liga.

Kutokana na uzito wa tukio hilo, Real Madrid imefungua uchunguzi wa kinidhamu dhidi yao.

CHUMBA CHA WACHEZAJI KUNA SHIDA

Siku hiyohiyo, saa chache baada ya tukio hilo, Kylian Mbappe alionekana akiondoka kwenye uwanja wa mazoezi wa Valdebebas huku akicheka, jambo lililoongeza lawama dhidi yake miongoni mwa mashabiki. Wiki iliyopita, Mbappe alikosolewa baada ya kuonekana akiwa mapumzikoni Italia badala ya kuuguza jeraha lake wakati Real Madrid ikicheza dhidi ya Espanyol.

Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya taarifa kudai alikuwa na ugomvi mkali na mmoja wa makocha wasaidizi wa kocha mkuu Alvaro Arbeloa. Mashabiki wengi sasa wamegeuka dhidi ya Mbappe huku kampeni za kumtaka aondoke zikiongezeka.

MARCA linadai baadhi ya nyota wa timu hawazungumzi kabisa ndani ya chumba cha kubadilishia nguo, huku wengine wakidaiwa kutokuwa tena na mawasiliano mazuri na kocha Arbeloa. Raul Asencio, Alvaro Carreras, Dani Carvajal na Dani Ceballos ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa na migogoro ya ndani msimu huu.

Carvajal anadaiwa kumuumiza mwenzake mazoezini kutokana na hasira za kukosa muda wa kucheza, huku Asencio, Carreras na Ceballos wakiachwa nje ya kikosi mara kadhaa kutokana na matatizo ya nidhamu.

REAL MADRID HAIFUNDISHIKI?

Kocha Arbeloa alipoteuliwa Januari mwaka huu akiwa na jukumu la kurejesha utulivu baada ya nusu ya kwanza ya msimu yenye vurugu chini ya Xabi Alonso. Watu wengi waliamini angeweza kuwadhibiti mastaa waliopo kikosini.

Hata hivyo, tangu Arbeloa afike, na timu kutolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kupoteza mbio za ubingwa, migawanyiko imeendelea kuongezeka.

Alonso alidaiwa kupoteza kabisa udhibiti wa chumba cha wachezaji, huku hasira za Vinicius Junior katika El Clasico ya Oktoba mwaka jana zikionyesha wazi hali mbaya ndani ya kikosi. Baada ya kuondoka, Alonso anaripotiwa kudai kuwa kikosi hicho “haiwezekani kukifundisha.”

Siku moja kabla ya ugomvi wa kwanza kati ya Valverde na Tchouameni, Carreras aliandika kwenye Instagram kwa njia ya mafumbo kuwa alipigwa kibao na Antonio Rudiger mazoezini. Wiki hii pia Mbappe anaripotiwa kugombana kwa maneno makali na mmoja wa makocha huku akionekana kujitenga zaidi ndani ya kikosi.

JINSI YA KUREJESHA NIDHAMU

Migogoro midogo mazoezini ni jambo la kawaida kwa wachezaji, lakini kinachoendelea Real Madrid kwa sasa siyo cha kawaida, kwani idadi ya matukio na migawanyiko haiwezi tena kufichwa kama sehemu ya ushindani wa ndani ya klabu.

Safari ya kesho kwenda Barcelona huku ubingwa ukiwa hatarini inaweza kuleta drama nyingine kwa mabingwa hao wa kihistoria wa Hispania. Kutokana na hali hiyo, Real Madrid inahitaji mabadiliko makubwa ya kiutamaduni mwishoni mwa msimu.

Arbeloa anatarajiwa kuondoka mwisho wa msimu, huku kocha mpya akipewa jukumu la kukiunganisha tena kikosi, kuwadhibiti nyota wenye mitazamo hasi na kurejesha mafanikio ndani ya timu.

Wakati Valverde na Tchouameni hawatarajiwi kuondoka, wachezaji wengine wenye matatizo kama Ceballos, Asencio na Carvajal wanaweza kuondolewa msimu ujao. Real Madrid pia inahitaji kuimarisha safu ya ulinzi wa kati na kiungo.

Lakini pamoja na lawama nyingi kuelekezwa kwa Mbappe, klabu haifikirii kumuacha. Badala yake, Real Madrid inataka kutafuta njia ya kumfanya nyota huyo wa Ufaransa acheze vizuri pamoja na mastaa wengine wa timu.

Dakika chache baada ya taarifa rasmi za Real Madrid kuhusu ugomvi huo, Valverde naye aliandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kueleza kilichotokea.

“Jana nilikuwa na tukio na mwenzangu kutokana na hali iliyotokea mazoezini,” aliandika Valverde kwenye Instagram.

“Uchovu wa mashindano na hasira hufanya mambo yaonekane makubwa zaidi.

“Katika vyumba vya kawaida vya wachezaji, mambo kama haya hutokea na mara nyingi yanamalizwa ndani kwa ndani bila kutoka nje. Lakini hapa kuna watu wanaosambaza uvumi, na kutokana na msimu huu bila mataji, kila kitu kinaonekana tatizo kubwa zaidi.

“Leo tulibishana tena. Wakati wa mabishano niligonga meza kwa bahati mbaya na kupata jeraha lililonifanya kwenda hospitali kwa uchunguzi.

“Mwenzangu Tchouameni hakunipiga, wala mimi sikumpiga yeye. Ninaumia sana kwa hali tunayoipitia.

“Kilichotokea ni mkusanyiko wa mambo mengi yaliyoishia kwenye mabishano yasiyo na maana. Nitaendelea kumtetea mwenzangu uwanjani kama kawaida.”