MAGEUZI YA SIMBA BARKER KULINDWA APEWA MUDA WA KUJENGA DOLA
UONGOZI wa Simba umeamua kubadili mtazamo wake katika uendeshaji wa benchi la ufundi kwa kuweka mkazo kwenye utulivu na mwendelezo, hatua inayolenga kuhakikisha makosa ya misimu iliyopita hayajirudii tena.
Baada ya kushuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha yaliyokuwa yakitikisa mipango ya timu, viongozi wa klabu hiyo sasa wamejipanga kumpa Kocha Mkuu, Steve Barker, muda wa kutosha kutekeleza majukumu yake na kujenga kikosi kulingana na falsafa yake ya soka.
Mkakati huo ni sehemu ya dira mpya ya Simba inayolenga kujenga mafanikio ya muda mrefu badala ya kufanya maamuzi ya haraka kila timu inapokumbana na changamoto. Uongozi unaamini kuwa mwendelezo wa benchi la ufundi ni moja ya nguzo muhimu za mafanikio ya kudumu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, tayari viongozi wa juu wamefikia mwafaka wa kuendelea kuwa na Barker hadi mwisho wa msimu ujao, wakiamini kuwa kocha huyo anahitaji muda wa kutosha ili kutekeleza kikamilifu mipango yake ya kiufundi na maendeleo ya timu.
Hatua hiyo inalenga kumpa Barker mazingira ya kazi yenye utulivu, tofauti na ilivyokuwa katika misimu ya nyuma ambapo mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha yalikwamisha utekelezaji wa baadhi ya mipango ya muda mrefu ya klabu.
Imeelezwa kuwa Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti Crescentius Magori, kwa kushirikiana na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji, imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuendeleza falsafa moja ya kiufundi badala ya kuanza upya kila baada ya muda mfupi kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Simba imepitia vipindi vya kubadilisha makocha mara kadhaa, hali iliyochangia kuyumba kwa baadhi ya malengo ya muda mrefu.
Moja ya matukio yaliyobaki kwenye kumbukumbu za mashabiki ni kuondoka kwa David Fadlu katikati ya msimu, jambo lililoilazimu timu kufanya marekebisho ya haraka katika hatua muhimu za mashindano.
Akizungumzia suala hilo, Magori alisema uzoefu walioupata kutokana na mabadiliko hayo umewapa somo kubwa, hivyo wameamua kujenga msingi wa utulivu kwa kumpa Barker nafasi ya kuendeleza kazi aliyoianza.
“Tumekuwa na mabadiliko ya makocha mara kadhaa katika misimu michache iliyopita.
Mara ya mwisho tulikutana na changamoto baada ya kuondoka kwa Fadlu katikati ya msimu. Tumepata funzo kutokana na hilo na sasa tuna Barker ambaye ameiongoza timu vizuri na ameonyesha uwezo mkubwa wa kuifikisha katika malengo yake,” amesema Magori.
Kwa sasa, Simba inaamini kuwa utulivu wa benchi la ufundi, sambamba na maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya kikosi, utakuwa silaha muhimu katika harakati za kupigania mataji ya ndani na kimataifa msimu ujao.
Mfumo huo mpya unatarajiwa kumpa Barker nafasi ya kutekeleza maono yake na kujenga Simba yenye ushindani wa kudumu kwa miaka ijayo.