Mshambuliaji Fiston Mayele ameandika historia mpya baada ya kujumuishwa katika kikosi cha mwisho cha timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2026.
Nyota huyo wa zamani wa Yanga na mshambuliaji wa sasa wa klabu ya Pyramids ya nchini Misri, anatarajiwa kuwa sehemu ya washambuliaji wa ‘The Leopards’ katika mashindano hayo makubwa duniani.
Hatua hii inajiri baada ya DR Congo kukata tiketi ya kihistoria kupitia bao la kichwa la dakika ya 100 lililofungwa na beki Axel Tuanzebe kwenye mchezo wa mwisho wa kufuzu dhidi ya Jamaica.
Ushindi huo uliamsha shangwe kubwa jijini Kinshasa na kuifanya nchi hiyo kuwa ya mwisho kabisa kukamilisha orodha ya timu 48 zitakazoshiriki fainali hizo. Hii ni mara ya kwanza kwa DR Congo kurejea kwenye Kombe la Dunia tangu mwaka 1974 waliposhiriki kwa mara ya kwanza kabisa wakiitwa Zaire.
Katika fainali hizo za mwaka 2026, DR Congo imepangwa katika Kundi K linalojumuisha mataifa makubwa ya Ureno, Colombia, na Uzbekistan. Kikosi hicho chini ya kocha Sébastien Desabre kimejaa mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa wanaocheza soka barani Ulaya pamoja na Uarabuni.
Kikosi kamili kilichotangazwa kocha huyo raia wa Ufaransa kupitia Shirikisho la Soka la DR Congo (FECOFA) ni makipa Timothy Fayulu (FC Noah), Lionel Mpasi (Le Havre) pamoja na kijana mdogo Mike Epolo (Standard Liege) kutoka nchini Ubelgiji.
Mabeki: Aaron Wan-Bissaka (West Ham United), Chancel Mbemba (Lille), Axel Tuanzebe (Burnley), Gédéon Kalulu (AEL Limassol), Joris Kayembe (Genk), Arthur Masuaku (Lens), Steve Kapuadi (Widzew Łódź), Rocky Bushiri (Hibernian), na Dylan Batubinsika (Larissa).
Viungo: Noah Sadiki (Sunderland), Edo Kayembe (Watford) Samuel Moutoussamy (Atromitos), Nathan Mukau (Lille), Charles Pickel (Espanyol), Ngal’ayel Mukau Mbuku (Montpellier), Brian Cipenga (Castellón), Théo Bongonda (Spartak Moscow) na mchezaji mkongwe Gaël Kakuta (Larissa).
Washambuliaji: Yoane Wissa (Newcastle United), Fiston Mayele (Pyramids), Cédric Bakambu (Real Betis), Simon Banza (Al Jazira), pamoja na Meschack Elia (Alanyaspor).