Nyota wa zamani wa Manchestsr United na England, Rio Ferdinand jana alianza rasmi ziara yake nchini kwa mapokezi makubwa huku akitoa ahadi ya kuhakikisha analisaidia soka la Tanzania kupiga hatua.
Ferdinand aliyewasili mnamo saa 5:00 asubuhi na kupokelewa na wadau wa soka na umati wa mashabiki ulioongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alisema ameshangazwa na mapokezo hayo na yamedhihirisha mapenzi ya Watanzania kwake na soka kijumla hivyo atasaidia juhudi za kuendeleza mchezo huo.
“Nina furaha sana. Hili ni jambo la ajabu kwangu kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kutembelea Tanzania na ninajivunia kuwa hapa.
“Watanzania wanapenda soka na ninafurahi kuona shauku waliyonayo kwa mchezo huu. Nitashirikiana na serikali na wadau wa soka kusaidia kuinua mchezo,” alisema Ferdinand.
Ferdinand aliongeza Tanzania inaonyesha maendeleo yanayotia moyo katika kukuza soka na kusisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa vijana wenye vipaji.
Pia alifichua alifanya mazungumzo na maafisa wa serikali kuhusu njia za kuimarisha maendeleo ya soka nchini.
“Ingawa nilistaafu kucheza, bado ni sehemu ya mfumo wa soka na nataka kuisaidia Tanzania kufikia mafanikio makubwa na kuwa nguvu kubwa katika soka,” alisema.
Akizungumza wakati wa mapokezi, Makonda alimshukuru Ferdinand kwa kukubali mwaliko wa serikali, akisema ziara hiyo imekuja wakati muhimu huku Tanzania ikiimarisha maandalizi ya kushirikiana kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027.
“Tunamshukuru Ferdinand kwa kukubali mwaliko wetu na kutembelea Tanzania. Uwepo wake utasaidia kukuza michezo na maendeleo ya soka nchini, sambamba na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Inatarajiwa Ferdinand atasafiri kwenda Dodoma kwa Treni ya Kisasa ya Umeme (SGR), ambako atahudhuria kikao cha Bunge kabla ya kwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na baadaye kutembelea miradi ya miundombinu ya AFCON 2027 jijini Arusha.