Habari za michezo

KUMEKUCHA MBEYA MPALAMO FESTIVAL, WADAU 2500 KUSHIRIKI

Vardo May 19, 2026 9:52 pm

JUMLA ya wadau wa utalii 2,500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kushiriki Mpalano Festival, linalotarajia kufanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 6 hadi 7 mwaka huu katika fukwe za Matema zilizopo wilyani Kyela mkoani Mbeya.

Tamasha hilo la msimu wa nne, linalenga kutangaza vivutio vya utalii, ngoma za asili na utamaduni, burudani, kuogelea, kupiga kasia, maonesho ya biashara, kufungua fursa za vijana na kuitangaza Wilaya ya Kyela.

Akizungumza leo Mei 19, 2026, mkurugenzi wa tamasha hilo Amos Asajile, amesema ikiwa ni msimu wa nne, wanatarajia wadau katika sekta mbalimbali kuonesha na kutangaza utalii wa ndani.

Amesema mbali na kutangaza vivutio, itakuwa sehemu ya fursa za kiuchumi kwa vijana kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Taifa akibainisha kuwa kupitia tamasha hilo wasanii wataonesha vipaji vyao na kujitangaza kama ilivyokuwa misimu mitatu nyuma.

“Tunatambua tamasha hili lina mchango mkubwa katika kukuza utalii wa kiutamaduni, kuinua wasanii wa ndani, kufungua fursa kwa vijana na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa Wilaya, Mkoa na Taifa.

“Kupitia tamasha hili watakuwapo pia wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi binafsi na za umma, ambao wote wataonesha bidhaa na huduma zao, hivyo kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja,” amesema Asajile.

Kwa upande wake mratibu wa tamasha hilo, Ipyana Mwakyusa, amesema kwa misimu mitatu nyuma wanajivunia kuwa sehemu ya wadau wa utalii kwa kutangaza vivutio na kufungua milango kwa wananchi kiuchumi.

Amesema mwaka huu tamasha hilo litakuwa na mabadiliko makubwa kwani changamoto zilizojitokeza nyuma wamezifanyia kazi akiwaomba wananchi, wadau kujitokeza kuunga mkono tukio hilo.

“Tunatarajia muitikio kuwa mkubwa kutokana na kilichoonekana mwaka jana, msimu huu tumejipanga vizuri na tuwakaribishe wadau kutuunga mkono ili kufikia malengo yetu,” amesema Mwakyusa.

AHADI YA RIO KWA SOKA LA TANZANIA KISA ENZO MARESCA, CHELSEA KUIBURUZA MAN CITY EPL