Habari za michezo
KISA ENZO MARESCA, CHELSEA KUIBURUZA MAN CITY EPL
Vardo
May 19, 2026
10:02 pm
CHELSEA ipo tayari kufungua mashtaka ya kisheria dhidi ya Manchester City kufuatia mienendo yao ya siri ya kumtaka aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Enzo Maresca, isipokuwa kama matajiri hao wa Manchester watakubali kulipa fidia kubwa.
Viongozi wa Chelsea wamechukizwa na taarifa za Maresca kufanya mazungumzo ya siri na Man City wakati bado akiwa anafanya kazi kama kocha mkuu wa klabu hiyo ya Stamford Bridge.
Maresca anatajwa kupewa nafasi kubwa ya kuziba pengo la Pep Guardiola atakayeondoka Man City baada ya mechi dhidi ya Aston Villa mwishoni mwa wiki hii.
Hata hivyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Man City endapo klabu hizo hazitafikia makubaliano ya kifedha. Chelsea imepanga kuwasilisha malalamiko kwenye uongozi wa Ligi Kuu ya England EPL ili uchunguzi wa kina uanze.
Mmoja wa wamiliki wa Chelsea, Behdad Eghbali, amefunguka kuhusu sakata hilo kwenye mkutano wa CAA World Congress of Sports na kukiri kuwa kuondoka kwa kocha huyo haikuwa mpango wa klabu hiyo ya Magharibi mwa London.
“Mabadiliko yale hayakuwa uamuzi wa klabu, kwa sababu ambazo siwezi kuzizungumzia sasa hivi kisheria. Nafikiri sababu zitakuwa wazi hivi karibuni. Lakini hayakuwa mabadiliko tuliyotaka kuyafanya.”
“Ni mabadiliko ambayo yameleta athari hasi kwenye msimu wetu, hasa unapobadilisha mifumo na wachezaji. Ni jambo ambalo inabidi tupambane ili tutoke hapa tulipo.” amesema kiongozi huyo
Kuondoka kwa Maresca kulikuja kama mshtuko mkubwa bila maelezo ya kina. Hata hivyo, taarifa za ndani zinafichua kuwa uhusiano kati ya Muitaliano huyo na mabosi wa Chelsea ulisambaratika kabisa tangu Desemba na kugeuka kuwa vita ya maneno.
Mambo yalianza kwenda mrama pale Maresca alipodai kuwa alipitia “saa 48 mbaya zaidi” Stamford Bridge kutokana na kukosa usaidizi kutoka kwenye uongozi baada ya kufungwa na Atalanta kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League).
Mbali na hayo, Maresca anadaiwa kupuuza ushauri wa idara ya matibabu ya klabu kuhusu muda wa kuwachezesha wachezaji uwanjani, kabla ya kuibuka kwa taarifa za siri kuwa alikuwa kwenye mazungumzo na klabu za Man City na Juventus ili ajiunge nazo.
Hata hivyo, wawakilishi wa Maresca wameshikilia msimamo wao na kusisitiza kuwa waliiarifu Chelsea mapema kuhusu uwepo wa mazungumzo hayo na klabu nyingine.
Baada ya vipigo mfululizo nyumbani dhidi ya Aston Villa na sare na Bournemouth kipindi cha Krismasi, Chelsea ilimfuta kazi Maresca Januari Mosi 2026 na kwa sasa inashika nafasi ya kumi na pointi 49 ikiwa imebaki michezo miwili.