MANCHESTER, ENGLAND: KATIKA wiki za hivi karibuni, Casemiro amekuwa kama anafanya ziara ya kuaga Ligi Kuu England na mechi ya Jumapili kati ya Manchester United na Nottingham Forest ilikuwa ya kipekee sana kwa Mbrazili huyo baada ya kushika kipaza sauti na kusema ‘kwaherini’.
Kiungo huyo alicheza mechi yake ya mwisho wa nyumbani Uwanja wa Old Trafford, Mei 17 na mashabiki wa Man United walimshangilia muda wote wa mechi, wakiimba jina lake na kumtaka aongeze mkataba wa ‘mwaka mmoja zaidi’ kwa shauku kubwa.
Hii huwa haifanyika mara nyingi, kuna wachezaji wengi wanaachana na timu kubwa lakini kitendo cha kuimbwa jukwaani kuwa wanamtaka aongeze mkataba wa mwaka mmoja ni kipya kwenye ulimwengu huu.
Hii ni Man United, timu kubwa Ulaya na duniani kwa jumla hivyo wameshapita mastaa wengi, lakini aga ya Casemiro ilionyesha picha ya tofauti.
Baada ya Michael Carrick kuichukua Man United, amesema baada ya kuingia aligundua kiungo huyo ni mchezaji muhimu sana kwenye timu hiyo, asiyependa kupoteza mechi yeyote hata kama ni ya kirafiki.
“Huyu ni mchezaji mkubwa, anapenda kuipambania timu hii na kwenye vyumba ni mtu muhimu, siyo muhimu kwa kuwa wachezaji wenzake wanamuogopa hapana, anajua kuzungumza kwa upole na kila mmoja, uwanjani na nje ya uwanja, mashabiki wanampenda kwa mengi, hajawahi kutupa karatasi ya shabiki anayetaka saini yake , inawezekana kuwa mengine mengi nje ambayo mimi siyafahamu,” amesema Carrick.
Kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid anatajwa kuwa kipenzi cha mashabiki wa Man United, amekuwa akishiriki kwenye matatizo yao moja kwa moja.
Kitu kimoja ambacho kinakumbukwa na wengi ni baada ya picha kuonekana akiwa hospitali alipokwenda kumsalimia shabiki mmoja wa United ambaye alikuwa mgonjwa, pia amekuwa akionekana mara kwa mara kwenye matatizo ya kijamii, kutembelea watoto, kukaa sehemu za kawaida kula, kuzungumza na hata kupiga picha na mashabiki bila majivuno mengi, hii inaweza kuwa sababu ya machozi ya mashabiki Old Trafford.
Hata hivyo, uamuzi wa kuachana naye tayari umefanywa.
Casemiro ataondoka klabuni mwishoni mwa msimu wakati mkataba wake utakapomalizika, hivyo kuhitimisha kipindi chake cha miaka minne England ambacho kilikuwa na mafanikio na changamoto mbalimbali, lakini kitakumbukwa kwa upendo na yeye pamoja na mashabiki wa United.
CASEMIRO ANAKWENDA WAPI?
Bado haijajulikana ni klabu gani itakuwa kituo chake kinachofuata. Kilicho wazi ni ataondoka Manchester United baada ya msimu wa 2025/26 kumalizika.
Inaonekana klabu yenye nafasi kubwa ya kumpata ni Inter Miami, mabingwa wa MLS Cup 2025. Ripoti zinaonyesha mchezaji huyo tayari amefanya mazungumzo na klabu hiyo kuhusu mkataba unaoweza kudumu hadi mwaka 2028.
Inter Miami, ambayo inamilikiwa kwa ushirikiano na nyota wa zamani wa Man United David Beckham, ilimleta Lionel Messi nchini Marekani mwaka 2023 na pia imewasajili mastaa wengine wa Ulaya kama Luis Suarez, Sergio Busquets, Jordi Alba na Rodrigo De Paul. Jarida la Forbes limeiweka Inter Miami kama klabu yenye thamani kubwa zaidi katika MLS mwaka huu ikiwa na thamani ya dola 1.35 bilioni .
Pia kuna taarifa kuwa Casemiro amepokea ofa kubwa kutoka klabu za Saudi Pro League kama Al Hilal na Al Nassr, anakocheza Cristiano Ronaldo, lakini inaelezwa Mbrazili huyo hana hamu ya kwenda Saudi Arabia kwa sasa.
JE ANAWEZA KUSTAAFU?
Hakuna dalili zozote zinazoonyesha kuwa Casemiro atastaafu soka mwaka huu baada ya kuondoka Man United.
Anatarajiwa kutajwa kuwa nahodha wa kikosi cha Brazil kitakachoshiriki Kombe la Dunia mwaka huu.
Pia, kiwango chake akiwa chini ya kocha Michael Carrick kimeonyesha bado ana uwezo mkubwa wa kuchangia uwanjani licha ya kuwa na umri wa miaka 34.
TAKWIMU ZAKE
Hadi tarehe 19 Mei 2026, Casemiro ameichezea Manchester United michezo 160 katika mashindano yote na kufunga mabao 26.
Ameisaidia klabu kushinda Kombe la EFL mwaka 2023, pamoja na FA Cup mwaka uliofuata.