Habari za michezo

MASTER MIND AVUNJA UKIMYA, AFICHUA UKWELI WA MALIPO YA ZIMBWE JR YANGA

Vardo May 19, 2026 3:49 pm

KUNA taarifa mpya na za ufafanuzi mzito kutoka kwa wakala wa mchezaji wa Yanga SC, Mohammed Hussein ‘Zimbwe JR’, Carlos Mastermind, ambaye amekanusha vikali uvumi uliosambaa mitandaoni ukidai kuwa nyota huyo anaidai klabu hiyo fedha.

Mastermind amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote na zimekusudiwa kupotosha umma, akisisitiza kuwa Yanga SC tayari imelipa asilimia 100 ya malipo ya awali ya kusaini mkataba (signing-on fee) pamoja na stahiki nyingine zote zilizokubaliwa kwenye makubaliano yao.

Amefafanua kuwa kwa sasa hakuna mgogoro wowote wa kifedha kati ya mchezaji huyo na klabu, na badala yake kila kitu kiko katika mfumo sahihi na wa kitaalamu kama ilivyokubaliwa awali.

Wakati huohuo, lengo kubwa kwa sasa ni kuhakikisha Tshabalala anarejea uwanjani akiwa katika ubora wake kamili ili aweze kuisaidia Yanga SC katika michezo muhimu iliyobaki ya msimu huu wenye ushindani mkubwa.

Kwa sasa, ‘Zimbwe JR’ anaendelea vyema na matibabu baada ya kupata majeraha katika mchezo dhidi ya Mbeya City FC uliochezwa katika dimba la KMC Complex, ambapo alianza kupatiwa huduma ya haraka mara baada ya tukio hilo.

Mastermind amesema nyota huyo ameendelea kuimarika hatua kwa hatua tangu alipoumia, ingawa bado hajafikia asilimia 100 ya utimamu wake wa kiafya.

Ameongeza kuwa amekuwa akipokea simu na ujumbe mwingi kutoka kwa mashabiki pamoja na vyombo vya habari vinavyotaka kujua maendeleo ya mchezaji huyo, hali iliyomlazimu kutoa ufafanuzi rasmi ili kuweka mambo sawa na kuondoa mkanganyiko.

“Mchakato wa matibabu unaendelea vizuri chini ya usimamizi wa madaktari, ambao wameridhishwa na mwenendo wa afya ya Tshabalala. Hii inatupa matumaini mapya kwa klabu na wapenzi wake,” amesema Mastermind.

NI HATARI TUPU KAPOMBE AREJEA WAKATI SIMBA IKIPIGANIA UBINGWA INTER MIAMI, SAUDI ARABIA ZAMNYATIA CASEMIRO