Habari za michezo

NI HATARI TUPU KAPOMBE AREJEA WAKATI SIMBA IKIPIGANIA UBINGWA

Vardo May 19, 2026 3:43 pm

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe, yupo tayari kuongoza kikosi hicho katika hatua za mwisho za msimu kwa lengo la kuhakikisha kinapata mafanikio makubwa katika mechi zilizosalia.

Ahmed amesema uzoefu pamoja na uongozi wa Kapombe ndani ya kikosi hicho ni silaha muhimu sana kwa Simba, hasa katika kipindi hiki ambacho ushindani wa mataji umefikia hatua ya juu na kila mchezo una uzito wa pekee.

Nahodha huyo alikosa mechi mbili za hivi karibuni, ikiwemo dhidi ya Mashujaa FC kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA United, kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.

Hata hivyo, sasa Kapombe ameripotiwa kuwa fiti na ameanza kurejea kikosini, hali inayoleta faraja kubwa kwa benchi la ufundi pamoja na mashabiki wa klabu hiyo wanaosubiri matokeo chanya kwenye mechi zijazo.

Ahmed amesema uwepo wa nahodha huyo uwanjani na hata kambini unawapa morali kubwa wachezaji wengine kuongeza juhudi na kupambana kwa nguvu zaidi kila wanapopata nafasi ya kuingia dimbani.

“Nahodha wetu Shomari Kapombe yupo tayari kuliongoza jahazi la Mnyama kumaliza msimu kwa mafanikio,” amesema Ahmed, akisisitiza kuwa kila mchezaji anatambua uzito wa mechi zilizobaki na umuhimu wa kupata matokeo.

Ameongeza kuwa Simba inaendelea na maandalizi ya kiwango cha juu kuhakikisha inakuwa katika ubora wake wa kawaida kwenye mechi muhimu za mwisho wa msimu, huku akipongeza mshikamano na nidhamu iliyooneshwa na wachezaji mazoezini.

YANGA YAPEWA ONYO JIPYA, SINGIDA BS WAPANGA KUENDELEA WALIPOISHIA DODOMA MASTER MIND AVUNJA UKIMYA, AFICHUA UKWELI WA MALIPO YA ZIMBWE JR YANGA