Habari za michezo
YANGA YARUDI KAMBINI KWA HASIRA, SINGIDA BLACK STARS KAZI WANAYO
Vardo
May 19, 2026
3:29 pm
BAADA ya kupata mapumziko mafupi kufuatia mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya JKT Tanzania, wachezaji wa Yanga SC wanarejea rasmi kambini leo kuanza maandalizi ya mchezo wao muhimu dhidi ya Singida Black Stars.
Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Ijumaa, Mei 22, 2026 katika Dimba la KMC Complex, Mwenge, macho ya mashabiki wengi yakielekezwa kwenye pambano hilo kutokana na umuhimu wake katika mbio za ubingwa.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya JKT Tanzania, wachezaji walipewa mapumziko mafupi kabla ya kurejea tena kambini na mazoezini leo.
Kamwe amesema kikosi hicho kitaweka kambi Avic Town, Kigamboni, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo ambao ameutaja kuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, Singida Black Stars.
“Leo timu inaingia kambini rasmi na tunaendelea na maandalizi kwa umakini mkubwa. Hatutaki kurudia makosa yaliyopita ya kupoteza pointi nyumbani.
Tunafahamu ugumu wa ligi, lakini wachezaji wetu wanaelewa majukumu yao ya kupambana katika kila hatua na kila mechi,” amesema Kamwe.
Amesisitiza kuwa msimu huu umefikia hatua ya maamuzi, hivyo timu inahitaji sapoti kubwa zaidi kutoka kwa mashabiki ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya msimu.
“Kwa sasa tunahitaji mashabiki wapambanaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Lengo letu la muda mfupi ni kuhakikisha hatupotezi alama dhidi ya Singida Black Stars Mei 22. Bado tuna michezo tisa mbele yetu, na hiyo ni vita ya kutetea mataji mawili ambayo yako mikononi mwa Yanga,” amesema Kamwe.