Habari za michezo

KASSALI ATUMA SALAMU KWA YANGA, SIMBA BADO INA NJAA YA MATAJI

Vardo May 19, 2026 3:21 pm

KIPA wa Simba SC, Djibrilla Kassali, amewapa matumaini mapya mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuahidi kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na taji la Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu.

Kauli ya Kassali imekuja katika kipindi ambacho ushindani wa Ligi Kuu umeingia hatua za mwisho zenye presha kubwa, huku kila timu inayowania ubingwa ikisaka ushindi katika kila mchezo uliosalia.

Kassali amesema anafurahishwa na namna mashabiki wa Simba wanavyoendelea kujitokeza kwa wingi uwanjani kuisapoti timu yao, jambo ambalo limekuwa chanzo cha hamasa kubwa kwa wachezaji ndani ya kikosi hicho.

Ameeleza kuwa sapoti wanayoipata kutoka kwa mashabiki ndiyo inayowapa nguvu ya kupambana hadi dakika ya mwisho katika kila mechi, akisisitiza kuwa uwepo wa mashabiki uwanjani umekuwa silaha muhimu kwa Simba katika kipindi hiki kigumu cha msimu.

Kipa huyo amesema kila mchezaji ndani ya kikosi anatambua ukubwa wa matarajio ya mashabiki wa Msimbazi, jambo linalowafanya kuongeza juhudi ili kuhakikisha hawawaangushi katika mbio za kuwania mataji.

“Nimefurahi sana kujitoa kwa mashabiki wa Simba. Wanakuja uwanjani na wanatuunga mkono, kitu ambacho kinatufanya tuwaahidi ubingwa msimu huu,” amesema Kassali.

Kauli hiyo imezua hamasa kubwa miongoni mwa mashabiki wa Simba ambao wanaendelea kuiunga mkono timu yao katika mbio za kuwania mataji msimu huu. Wengi wanaamini morali ya wachezaji imeongezeka kutokana na ushindani mkubwa uliopo ligi.

Katika kipindi hiki cha lala salama ya msimu, kila mchezo kwa Simba unaonekana kama fainali, inayowalazimu wachezaji kuongeza umakini na kujituma zaidi ili kuhakikisha wanabaki kwenye mbio za ubingwa hadi mwisho wa msimu.

Kwa sasa, Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 52, nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 54.

TANO LIGI KUU WANAWAKE KUPIGWA LEO YANGA YARUDI KAMBINI KWA HASIRA, SINGIDA BLACK STARS KAZI WANAYO