BAADA ya jana kupigwa mechi moja ya Ligi ya Wanawake Tanzania (TWPL) kati ya mabingwa watetezi, JKT Queens dhidi ya Tausi FC, leo ligi hiyo itaendelea zikipigwa mechi tano za raundi ya 17.
Vinara wa ligi hiyo, Simba Queens watakuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuikaribisha Ruangwa Queens katika mechi inayotarajiwa kuwa na umuhimu kwa wenyeji wanaotaka kuendelea kuongoza msimamo wa ligi.
Timu hiyo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa katika kiwango bora baada ya kucheza mechi 16 bila kupoteza.
Yanga Princess inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo, itakuwa mwenyeji wa Ceasiaa Queens kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam mechi itakayopigwa saa 12 jioni.
Yanga Princess inapewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini itahitaji kuwa makini dhidi ya wapinzani wao wanaopambana kujinasua kutoka chini.
Alliance Girlsitasafiri hadi Karume mkoani Mara kuvaana na Bunda Queens katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Michezo mingine ya raundi hiyo itawakutanisha Fountain Gate Princess dhidi ya Mashujaa Queens kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, huku Bilo FC ikicheza na Geita Queens kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema wanafahamu ugumu wa kucheza na timu iliyopo kwenye presha ya kushuka daraja. “Ni ngumu sana kwa sababu na wao watakuja kutushambulia ili angalau wapate pointi, tumejiandaa vizuri na tunaamini kile tulichodhamiria msimu huu kitaenda kufanikiwa.”
Kocha wa Ceasiaa, Sultan Juma, amesema: “Kuna ugumu wa kucheza na hizi timu kubwa lakini sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata pointi tatu na kukaa kwenye nafasi nzuri ya msimamo.”