Habari za michezo
BAADA YA MIAKA 13 MWAMBA ANAREJEA REAL MADRID
Vardo
May 19, 2026
9:06 am
MADRID, HISPANIA: KOCHA maarufu raia wa Ureno, Jose Mourinho, amekubali kurejea kuinoa Real Madrid baada ya miaka 13 tangu kuondoka kwake kwa mazingira yaliyogubikwa na migogoro ndani ya klabu hiyo.
Mourinho, ambaye kwa sasa ni kocha wa Benfica nchini kwao Ureno, anatarajiwa kurejea katika dimba la Santiago Bernabeu kwa mkataba wa miaka miwili, licha ya upinzani mkali kutoka kwa nyota wa zamani wa timu hiyo, Iker Casillas ambaye amesema hadharani kuwa hataki kocha huyo afundishe Madrid.
Casillas, aliyewahi kuondolewa kwenye nafasi ya kipa namba moja na Mourinho wakati wa utawala wake wa kwanza Madrid, hakuficha hisia zake kupitia mtandao wa X.
“Sina tatizo binafsi na Mourinho. Ni kocha mkubwa mwenye uwezo wa hali ya juu, lakini sitaki arudi Real Madrid. Nafikiri kuna makocha wengine wanaofaa zaidi kuiongoza klabu ninayoipenda,” aliandika Casillas.
Mourinho mwenye umri wa miaka 63, anarejea Madrid katika kipindi kigumu ambapo klabu hiyo imekumbwa na migogoro ya wachezaji, kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushuhudia Barcelona wakitwaa ubingwa wa LaLiga kwa kishindo.
Taarifa zinaeleza kuwa kocha huyo atasafiri kwenda Madrid baada ya mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Athletic Bilbao ili kukamilisha makubaliano rasmi ya kuichukua timu hiyo.
Habari za kurejea kwake zimeibuka baada ya Benfica kumaliza msimu wa Ligi Kuu Ureno bila kupoteza mchezo wowote, kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Estoril.
Baada ya mchezo huo, Mourinho alikiri kuwa hatma yake itaamuliwa ndani ya wiki hii.
“Nahitaji muda na nafasi ya kufanya maamuzi. Wiki hii itakuwa muhimu sana kwangu,” alisema Mourinho.
Ingawa alikanusha kuwa hajazungumza moja kwa moja na Madrid, taarifa zinaeleza wakala wake Jorge Mendes ndiye anayesimamia mazungumzo hayo.
Ripoti pia zimebainisha kuwa kuna kipengele kwenye mkataba wake kinachoruhusu Madrid kulipa kiasi cha pauni 2.6 milioni ili kuvunja mkataba wake na Benfica ndani ya siku 10 baada ya msimu kumalizika.
Mourinho aliwahi kuinoa Real Madrid kati ya mwaka 2010 hadi 2013 na kuipa taji moja la LaLiga, Copa del Rey pamoja na Kombe la Hispania huku akipambana vikali na Barcelona ya kocha Pep Guardiola.
Awali, Madrid ilimfuta kazi kocha Xabi Alonso baada ya miezi minane pekee, kabla ya Alvaro Arbeloa kupandishwa kutoka timu B ya klabu hiyo kuongoza kikosi cha wakubwa lakini anaonekana kushindwa kuendana na kasi kubwa iliyopo kwa sasa.
Mbali na changamoto za uwanjani, Mourinho anakutana na mazingira yenye migogoro mikubwa ndani ya kikosi hicho. Kiungo Federico Valverde anaripotiwa kufikishwa hospitali baada ya ugomvi na Aurelien Tchouameni, huku pia Antonio Rudiger na Alvaro Carreras wakitajwa kuhusika kwenye vurugu nyingine kambini.
Wakati huohuo, mshambuliaji nyota Kylian Mbappe alizua mjadala mpya baada ya kudai kuwa aliambiwa yeye sasa ni chaguo la nne katika safu ya ushambuliaji ya Madrid, huku mashabiki wakipiga kura ya kutomtaka staa huyo kwenye kikosi hicho.
Hata hivyo, imaaminika kuwa Mourinho ndiye kocha sahihi kwenye kikosi hicho kwa sasa kutokana na misimamo na mafanikio makubwa ambayo anayo kocha huyo wa zamani wa Porto ya Ureno.
Kocha huyo amefanikiwa kutwaa makombe makubwa akitwaa Ligi ya Mabingwa mara mbili akiwa na Inter Milan pamoja na Porto, huku akifanikiwa kutwaa ubingwa wa Europa akiwa na Man United, jumla amefanikiwa kutwaa makombe 20 akiwa kocha mkuu katika timu sita alizofundisha.