WAKATI droo ya mashindano ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ikipangwa kufanyika leo jijini Cairo, Misri, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imetamba kuwa inatamani kupangwa katika kundi lenye timu bora zaidi katika mashindano hayo.
Mkurugenzi wa timu za taifa za Tanzania, Almas Kasongo, alisema sababu ya Taifa Stars kuhitaji kukutana na wapinzani imara zaidi katika mechi hizo za kufuzu ili timu hiyo iimarike zaidi kabla ya Fainali za AFCON 2027.
Kasongo alisema pamoja na uhakika wa Taifa Stars kushiriki fainali hizo kwa vile Tanzania ni miongoni mwa wenyeji watatu wa AFCON 2027, timu hiyo inayapa uzito mkubwa mashindano hayo ya kufuzu na itakuwa tayari kupangwa dhidi ya mpinzani yeyote.
“Tunajipanga kuipokea droo kwa vyovyote itakavyokuja. Sisi kwa upande wetu tunatamani kupangwa katika kundi na timu ngumu na bora. Ni kitu ambacho kitatufanya tupate uzoefu na ufiti wa mashindano. “Siku zote unapaswa kuwa na ugumu katika maandalizi ili iwe rahisi katika mashindano. Hivyo sisi tuko tayari na ndio kama nilivyokuambia kwamba tukiwa katika kundi gumu itatusaidia kujenga timu yetu,”.
Kasongo alisema benchi la ufundi la Taifa Stars na uongozi wa TFF watahakikisha timu inacheza mashindano hayo kwa kushindana na sio kubweteka kwa vile imeshafuzu.
“Kitu kikubwa kinachotakiwa kwa wachezaji na benchi la ufundi ni kuishi kiweledi. Hatupaswi kuwa katika hali ya kuridhika kwamba tumeshafuzu na badala yake tunapaswa kuyapa uzito mashindano haya,” alisema Kasongo.
Droo hiyo itaanza saa 9:00 alasiri kwa muda wa Afrika Mashariki itachezwa na wachezaji nyota wa zamani wakiongozwa na Troost-Ekong (Nigeria), Gradel (Ivory Coast), El Hadary (Misri), na Tresor Mputu (DR Congo).
Taifa Stars itakuwa katika chungu cha tatu kati ya timu 48.
Makundi 12 yenye timu nne kila moja, yatapangwa katika droo hiyo ambapo kila kundi litakuwa na timu moja moja kutoka katika vyungu vinne. Timu zilizo katika chungu kimoja hazitopangwa katika kundi moja.