Habari za michezo
YANGA YAPEWA ONYO JIPYA, SINGIDA BS WAPANGA KUENDELEA WALIPOISHIA DODOMA
Vardo
May 19, 2026
3:38 pm
AFISA Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, ameonyesha kujiamini kuelekea mchezo wao mkubwa dhidi ya Yanga SC, akisema mabingwa hao wa Tanzania Bara wanapaswa kuwa makini kwani wanaweza kukumbana na yaliyoikuta timu hiyo mbele ya Dodoma Jiji FC hivi karibuni.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuchezwa Ijumaa Mei 22, 2026 katika dimba la KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, huku ukiwa miongoni mwa mechi zinazotarajiwa kuvuta hisia kubwa za mashabiki kutokana na ushindani mkali wa msimu huu.
Singida Black Stars wataingia katika pambano hilo wakiwa wageni, huku kikosi hicho kikitarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo kikitokea Tanga kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na Yanga.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Massanza alisema wanautambua ubora na uzoefu wa wapinzani wao, lakini hilo haliwapunguzi morali kwani wanaamini kikosi chao kina uwezo wa kufanya matokeo makubwa.
Amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wana ari kubwa ya kupambana.
“Hii ni mechi kubwa sana na tunajua tunaenda kucheza dhidi ya timu yenye ubora mkubwa. Lakini soka la sasa haliwezi kutabirika kirahisi, kila timu inapambana kupata matokeo na hilo linaongeza ushindani mkubwa kwenye ligi,” amesema Massanza.
Afisa huyo aliikumbushia mechi ya hivi karibuni ambayo Dodoma Jiji FC ilifanikiwa kupata matokeo mbele ya Yanga, akisema hilo linaonyesha wazi kuwa hakuna timu isiyoweza kufungwa katika mazingira ya sasa ya ushindani wa ligi.
Kwa mujibu wake, matokeo hayo yanawapa matumaini na kuamini kuwa nao wana nafasi ya kufanya jambo maalum mbele ya mabingwa hao.
“Juzi tulicheza dhidi ya Dodoma Jiji FC kwenye uwanja wetu wa Airtel mjini Singida na wakaonyesha kwamba mpira wa sasa una ushindani mkubwa. Kilichowatokea Yanga kinaweza kujirudia tena kama tutatumia vizuri nafasi zetu,” ameongeza.
Massanza amesema benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa Singida Black Stars wameuchukulia mchezo huo kama nafasi muhimu ya kuonyesha uwezo wao dhidi ya moja ya timu bora nchini.
Amesisitiza kuwa katika soka hakuna lisilowezekana, hivyo wanaingia dimbani wakiwa na lengo la kupambana kwa nguvu zote na kuondoka na matokeo chanya.