Habari za michezo

DODOMA JIJI WAJIPANGA KUKABILIANA NA HASIRA YA SIMBA

Vardo May 23, 2026 9:40 am

WAKATI presha ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiendelea kupanda kila siku, Simba SC wamehamishia nguvu na akili zao zote kwenye mchezo wao wa kesho Jumapili dhidi ya Dodoma Jiji FC, huku uongozi wa klabu hiyo ukiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa KMC Complex kuipa sapoti timu yao.

Kupitia Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, mashabiki wa timu hiyo maarufu kama “Wana Lunyasi” wamehamasishwa kuijaza KMC Complex ili kuwapa morali wachezaji katika mchezo huo muhimu wa kuwania pointi tatu.

Ahmed amesema kwa sasa ndani ya Simba hakuna jambo lingine linalopewa kipaumbele zaidi ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, timu ambayo imekuwa ikitoa ushindani mkubwa dhidi ya vigogo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Akili yetu yote ipo kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Dodoma Jiji. Tunafahamu ubora wao, ugumu wao na namna wanavyocheza kwa ushindani mkubwa, hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kujitoa kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Ahmed.

Ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu, kila mchezo una uzito mkubwa kwa Simba kutokana na ushindani mkali wa kuwania ubingwa, jambo linaloifanya timu hiyo kuhitaji ushindi katika kila mechi iliyobaki.

Ahmed amewataka viongozi wa matawi pamoja na makundi mbalimbali ya mashabiki kuendelea kuhamasishana ili kuhakikisha idadi kubwa ya mashabiki inafika uwanjani kuisapoti timu katika hatua hii muhimu ya msimu.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na rekodi ya Dodoma Jiji ya kuzisumbua timu kubwa za Kariakoo, huku Simba wakihitaji ushindi ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

JANGWANI KUNA PESA, WAJANJA WANAICHUKUA FURSA SASA HIVI PACOME AWAACHIA YANGA KIGUGUMIZI