Habari za michezo

PACOME AWAACHIA YANGA KIGUGUMIZI

Vardo May 23, 2026 9:43 am

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, amezua taharuki kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kupata majeraha katika eneo la juu ya goti na kushindwa kuendelea na mchezo wa jana dhidi ya Singida BS.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida BS, lakini furaha ya ushindi huo ilifunikwa na wasiwasi juu ya hali ya nyota huyo muhimu wa kikosi hicho.

Pacome alilazimika kutolewa mapema baada ya kuonekana kushindwa kuhimili maumivu hayo, hali iliyowaacha mashabiki pamoja na benchi la ufundi wakiwa na hofu ya kumpoteza mchezaji huyo kuelekea michezo ya mwisho ya msimu.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe, imeelezwa kuwa vipimo vya awali vinaonyesha majeraha hayo si makubwa sana, ingawa bado kuna umuhimu wa kufanyika uchunguzi wa kina kubaini ukubwa halisi wa tatizo hilo.

Kamwe amesema Pacome anatarajiwa kufanyiwa vipimo zaidi leo asubuhi ili kupata majibu sahihi yatakayobainisha kama ataendelea kucheza katika ratiba zijazo za timu hiyo au atahitaji muda wa kuwa nje ya uwanja.

Mashabiki wa Yanga wameonekana kuguswa na taarifa hiyo, huku wengi wakimtumia salamu za pole na kumuombea apone haraka kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya kikosi hicho msimu huu.

Pacome ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa Yanga kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kufunga mabao na kubadili matokeo ndani ya muda mfupi, jambo linaloufanya uwepo wake kuwa muhimu sana kwa mafanikio ya timu hiyo.

DODOMA JIJI WAJIPANGA KUKABILIANA NA HASIRA YA SIMBA BONUS ZA CAF ZATUA LIGI KUU KWA MASTAA WA YANGA