Habari za michezo
SERENGETI BOYS NA MATUMAINI KIBAO
Vardo
May 23, 2026
10:15 am
NYOTA wa timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17, Serengeti Girls, wamesema wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri mbele ya mashabiki wao kuelekea mzunguko wa kwanza wa raundi ya pili ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Afrika Kusini.
Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa Mei 23, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 12 jioni kabla ya marudiano kufanyika Mei 31, 2026 Afrika Kusini.
Nyota wa kikosi hicho, Harrier Juma amesema kucheza nyumbani kunawapa hamasa kubwa ya kupambana na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kabla ya mechi ya marudiano.
“Kitu ambacho kinatupa morali ni tupo uwanja wa nyumbani, tutakuwa na faida ya mashabiki watakaotupa motisha kubwa. Tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili watupe sapoti,” amesema Harrier.
Golikipa wa timu hiyo, Nusra Jaffar, ambaye amesema uwepo wa mashabiki utakuwa chachu ya wachezaji kuonyesha kiwango bora dhidi ya wapinzani wao.
“Nategemea kuona sapoti kubwa ya mashabiki kwenye mechi yetu hii, sapoti yenu ni muhimu kwetu. Tunawaahidi tutaonyesha kiwango bora,” amesema Nusra.
Serengeti Girls inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa baada ya kuiondosha Botswana katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-2. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Francistown, Tanzania ilishinda mabao 3-2 kabla ya kukamilisha kazi nyumbani kwa ushindi wa mabao 3-0.
Katika michezo hiyo, kikosi hicho kilionyesha ubora mkubwa wa ushambuliaji pamoja na nidhamu ya mchezo, mambo yaliyowapa nafasi ya kusonga mbele kwa kujiamini.
Kwa upande wa Afrika Kusini, timu hiyo ilitinga moja kwa moja raundi ya pili baada ya wapinzani wao wa raundi ya kwanza, Jamhuri ya Afrika ya Kati, kujiondoa kwenye mashindano.
Mashindano ya Kombe la Dunia kwa wasichana U-17 yanatarajiwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Oktoba 17 hadi Novemba 7 mwaka huu, huku Afrika ikipewa nafasi tano ikiwemo wenyeji Morocco.
Iwapo Serengeti Girls itafanikiwa kufuzu, itakuwa ni mwendelezo wa mafanikio kwa soka la vijana Tanzania baada ya Tanzanite Queens kufuzu Kombe la Dunia U-20 nchini Poland, sambamba na Timu ya Taifa ya wavulana U-17 kufuzu michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar.
Serengeti Girls pia itakuwa ikirejea kwenye historia yake nzuri ya mwaka 2022 ilipofika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia lililofanyika nchini India.