Habari za michezo

NEUER, MUSIALA, WIRTZ WABEBA TUMAINI LA UJERUMANI

Vardo May 23, 2026 10:23 am

BERLIN, UJERUMANI: KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann ametangaza rasmi kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 26 kitakachoiwakilisha nchi hiyo katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 huku taarifa iliyovutia wengi ikiwa ni kurejea kwa golikipa mkongwe Manuel Neuer ambaye alikuwa ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya Euro 2024.

Wadau wengi waliamini safari ya Neuer kuitumikia Ujerumani ilikuwa imefikia mwisho, lakini mlinda mlango huyo mwenye miaka 40 amerejea baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Bayern Munich msimu huu, hasa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Nagelsmann ameweka wazi kuwa Neuer si sehemu tu ya kikosi hicho bali ndiye golikipa namba moja kuelekea mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.

Nagelsmann alisema waliwasiliana mapema na Neuer na kumuuliza kama alikuwa tayari kurejea kuitumikia nchi yake kwa mara nyingine. Kwa mujibu wa kocha huyo, Neuer alionyesha hamu kubwa ya kurejea.

Kocha huyo alikiri uamuzi huo huenda uliwaumiza baadhi ya makipa wengine waliokuwa wakitajwa kuchukua nafasi yake, hasa Oliver Baumann wa Hoffenheim, lakini akasisitiza kuwa uamuzi huo ulitokana na tathmini ya kiufundi na uzoefu mkubwa wa Neuer.

Mbali na uwezo wake wa kuokoa mipira, Neuer anabeba historia kubwa ndani ya soka la Ujerumani, akiwa mmoja wa viongozi waliowahi kusaidia taifa hilo kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Nagelsmann na Neuer waliwahi kuwa na tofauti walipokuwa Bayern Munich, lakini kuelekea Kombe la Dunia wawili hao wameonekana kuweka pembeni tofauti zao kwa lengo moja la kuirudisha Ujerumani kwenye ubora wake.

Mbali na habari ya Neuer, macho mengi pia yameelekezwa kwa kinda mwenye miaka 18, Lennart Karl ambaye amepewa nafasi kubwa katika kikosi hicho.

Karl ni mmoja wa vijana wanaotabiriwa kuwa na mustakabali mkubwa kwenye soka la Ujerumani. Tayari ameonyesha uwezo mkubwa akiwa Bayern Munich huku akivutia kwa utulivu na uwezo wa kucheza chini ya presha.

Kiungo wa Borussia Dortmund, Felix Nmecha naye amerejea baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimsumbua. Nagelsmann anaamini ana uwezo wa kuwa mmoja wa viungo bora duniani.

Katika safu ya ushambuliaji, Ujerumani itategemea ubora wa mastaa wake vijana kama Jamal Musiala, Florian Wirtz, Kai Havertz pamoja na Leroy Sane.

Musiala amepewa nafasi licha ya kutokuwa amecheza mechi za timu ya taifa tangu mapema mwaka 2025 kutokana na majeraha, huku Sane akiendelea kuaminiwa kutokana na uzoefu wake wa mashindano makubwa.

Kiungo Nadiem Amiri, Jamie Leweling, Angelo Stiller pamoja na Nathaniel Brown pia wameitwa, huku majina kama Niclas Fullkrug, Tom Bischof na Said El Mala yakikosa nafasi jambo lililowashangaza mashabiki wengi.

KIKOSI KILIVYOTANGAZWA

Tangazo la kikosi hicho limekuja kwa mtindo tofauti ukilinganisha na Euro 2024 ambapo safari hii Ujerumani walitumia video maalum zilizohusisha ndugu, marafiki pamoja na jumbe za motisha kutoka kwa Nagelsmann kwa baadhi ya wachezaji walioteuliwa.

Maandalizi rasmi ya Ujerumani yataanza mwishoni mwa mwezi huu kwa kambi maalum kabla ya kuelekea Marekani. Kai Havertz atajiunga baadaye kutokana na majukumu ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Arsenal.

Ujerumani watacheza mechi za kirafiki dhidi ya Finland Mei 31 mjini Mainz na Marekani Juni 6 Chicago kabla ya kuanza kampeni ya Kombe la Dunia Juni 14 dhidi ya Curacao huko Houston.

HII NI MIAMBA

Kwa miaka mingi, Ujerumani wamejenga utamaduni wa ushindi unaotokana na nidhamu, moyo wa kupambana na uwezo mkubwa wa kushughulikia presha za mashindano makubwa.

Ni moja ya mataifa yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia ikiwa imetwaa ubingwa mara nne. Safari yao ya mafanikio ilianza rasmi mwaka 1954 walipotwaa ubingwa wao wa kwanza nchini Uswisi katika mechi maarufu iliyojulikana kama “Muujiza wa Bern” baada ya kuifunga Hungary mabao 3-2.

Miaka ya 1970 ilileta kizazi cha Franz Beckenbauer kilichowapa ubingwa mwingine mwaka 1974 dhidi ya Uholanzi ya Johan Cruyff.

Mwaka 1990, Ujerumani walitwaa ubingwa wao wa tatu baada ya kuifunga Argentina bao 1-0 katika fainali, huku kizazi cha Lothar Matthaus, Jurgen Klinsmann na Rudi Voller kikitamba.

Mwaka 2006 walipoandaa Kombe la Dunia nyumbani, kizazi kipya cha Thomas Muller, Toni Kroos, Philipp Lahm pamoja na Neuer kilianza kuonekana.

7-1 ILIYOITIKISA DUNIA

Kombe la Dunia la mwaka 2014 nchini Brazil likawa kilele cha mafanikio hayo. Ujerumani walitinga fainali baada ya kuifunga Brazil mabao 7-1 katika nusu fainali, matokeo yaliyotikisa dunia ya soka.

Katika fainali dhidi ya Argentina, Mario Gotze alifunga bao la ushindi na kuipa Ujerumani taji lao la nne la dunia.

Hata hivyo, baada ya mafanikio hayo, mambo yalibadilika ghafla. Katika Kombe la Dunia 2018 nchini Russia pamoja na 2022 Qatar, Ujerumani waliondolewa mapema jambo lililozua maswali mengi kuhusu mustakabali wa soka lao.

Sasa matumaini yanaelekezwa kwa kizazi kipya kinachoongozwa na Musiala, Wirtz, Havertz pamoja na kurejea kwa Neuer.Nagelsmann anaonekana kujenga timu yenye uwiano wa vijana wenye vipaji vikubwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa, huku historia ya Ujerumani ikiendelea kuonyesha jambo moja muhimu, huwezi kuibeza timu hiyo inapofika kwenye mashindano makubwa.

SERENGETI BOYS NA MATUMAINI KIBAO NI VITA NUSU FAINALI FA PEMBA