SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMS) imesema itaweka bei elekezi juu ya matumizi ya viwanja vya Wilaya na Mkoa vinavyoendelea kujengwa kisiwani hapa ili kuwaondolea usumbufu na kuwapunguzia gharama wananchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub kwa niaba ya Waziri Riziki Pembe Juma katika Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Amesema, kwasasa timu zinatozwa Sh150,000 kwa mechi za mchana na Sh200,000 usiku na Wizara imebaini sio wote wenye uwezo wa kumudu gharama hizo.
“Licha ya Serikali kuingia makubaliano ya viwanja vya Mkoa na Wilaya kumpa Mwendeshaji Bahari Leisure, Wizara itakuja na bei elekezi itakayotoa kwa ajili ya wananchi kuweza kutumia viwanja hivyo na kuibua vijapji,” amesema.
Alisisitiza Wizara imepanga kuweka bei elekezi zitakazozingatia hali halisi ya watumiaji ili kuhakikisha gharama zinabaki kuwa nafuu kwa watumiaji huku zikiwezesha uendeshaji endelevu wa viwanja hivyo.
Gulam amesema Wizara hiyo ina mpango wa kutoa bure uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, kwa timu za vijana kwa siku za Jumamosi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana ili wananchi wafaidi matunda ya serikali.
Aidha, amesema Serikali haina dhamira ya kubadilisha viwanja hivyo kuwa biashara pekee, bali kuhakikisha vinatumika kwa manufaa mapana ya jamii.
Amesema, madhumuni makuu ya ujenzi wa viwanja hivyo ni kutambua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo, pamoja na kuimarisha afya za wananchi.