Habari za michezo

WPL KUNA MECHI MBILI ZA UAMUZI

Vardo May 23, 2026 10:02 am

RAUNDI ya 18 ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) itaendelea Jumamosi hii Mei 23, 2026 kwa mechi sita kupigwa, lakini macho ya wengi yataelekezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam ambapo vinara wa ligi hiyo, Simba Queens watavaana na mabingwa watetezi JKT Queens katika mechi inayoweza kuamua mwelekeo wa mbio za ubingwa msimu huu.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hadi sasa, Simba Queens inaongoza ikiwa na pointi 49 baada ya kucheza mechi 17, ikifuatiwa na JKT Queens yenye pointi 42 katika idadi hiyo hiyo.

Mechi hiyo inatajwa kuwa ya uamuzi kwa pande zote mbili, hasa kwa JKT Queens ambayo inahitaji ushindi ili kupunguza tofauti ya pointi na kuendelea kuwa hai kwenye mbio za kutetea taji lao.

Iwapo JKT Queens itaibuka na ushindi, itafikisha pointi 45 na kupunguza gepu la pointi hadi nne pekee dhidi ya Simba Queens, jambo litakaloongeza presha kubwa kwenye mbio za ubingwa huku zikiwa zimesalia raundi chache kuelekea mwisho wa msimu.

Hata hivyo, Simba Queens ina nafasi nzuri zaidi ya kuukaribia ubingwa. Endapo itaibuka na ushindi dhidi ya JKT Queens, itafikisha pointi 52 na kuhitaji kushinda mechi mbili pekee kati ya tano zitakazosalia ili kutangaza ubingwa rasmi wa ligi hiyo.

Mara ya mwisho zilipokutana timu hizo Januari 8 mwaka huu, Simba ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya 1-1 mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mbali na pambano hilo kubwa, mechi nyingine yenye mvuto ni kati ya Ruangwa Queens dhidi ya Tausi FC itakayopigwa Uwanja wa Majaliwa.

Ruangwa Queens inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa nafasi ya 11 na pointi tisa, huku ikihitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kubaki ligi kuu msimu ujao.

Kwa upande wa Tausi FC, iliyopo nafasi ya saba na pointi 19, inahitaji matokeo mazuri ili kujiweka salama zaidi dhidi ya hatari ya kushuka daraja.

Mechi zingine za raundi hiyo, Mashujaa Queens itaikaribisha Yanga Princess kwenye Uwanja wa TFF Kigamboni, Bunda Queens itacheza dhidi ya Bilo Queens mjini Mara, huku Fountain Gate Princess ikiminyana na Ceasiaa Queens kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

Geita Queens nao watakuwa nyumbani kuikaribisha Alliance Girls kwenye Uwanja wa Nyankumbu.

Akizungumzia mechi yao dhidi ya Ruangwa Queens, Kocha Mkuu wa Tausi, Martin Hammel amesema: “Tunafahamu tunaenda kucheza na timu ambayo haijafanya vizuri, hivyo watakuja kujaribu kushambulia ili angalau wapate pointi, sisi pia tumejipanga kuchukua pointi hizo ingawa haitakuwa rahisi.”

Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema: “Kama ilivyo kauli mbiu yetu ‘Nguvu Moja’ tunaenda kupambania pointi tatu ngumu zingine dhidi ya mpinzani mgumu, haitakuwa mechi rahisi lakini tunaamini kwa maandalizi tuliyoyafanya yataenda kutupa matokeo mazuri.”

KAGERA SUGAR, GEITA GOLD KATIKA VITA YA KILELENI CHAMPIONSHIP SMS YATOA TAMKO MATUMIZI YA UWANJA