Geita ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Timu hiyo inayofundishwa na Kocha, Zubery Katwila aliyejiunga nayo akitokea Bigman FC, anaipambania kuirejesha Ligi Kuu Bara kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kuzifundisha pia, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar.
Mechi nyingine za leo itashuhudiwa Hausung FC iliyotoka kuchapwa mabao 3-0, ugenini dhidi ya Bigman FC ikirejea kwenye Uwanja wa Amani uliopo mjini Njombe kwa kuikaribisha B19 FC, yenye kumbukumbu nzuri baada ya kuichapa Mbeya Kwanza 1-0.
KenGold baada ya kuchapwa mabao 3-1, dhidi ya Polisi Tanzania mechi ya mwisho, inarejea kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya jijini, Mbeya kuikaribisha Songea United, iliyotoka pia kupoteza Tanga kwa kufungwa na African Sports mabao 3-0.
Kwenye Uwanja wa Sheikh, Amri, Abeid, jijini, Arusha kutakuwa na ‘Derby ya Monduli’, ambapo Mbuni FC iliyotoka kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya Kagera Sugar itapambana na majirani zao wa TMA FC, iliyochapwa pia na Geita Gold ugenini mabao 4-0. Baada ya Mbeya Kwanza kushangazwa na B19 FC kwa kuchapwa bao 1-0, mechi iliyopita jijini, Dar es Salaam, inarudi kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini, Tabora kwa kuikaribisha Bigman FC ya Lindi, iliyotoka kuichapa Hausung FC mabao 3-0.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, African Sports baada ya kuichapa Songea United mabao 3-0, itaikaribisha maafande wa Polisi Tanzania iliyoichapa KenGold ya Mbeya 3-1, huku Barberian ikicheza dhidi ya kikosi cha maafande wa Transit Camp.
Barberian iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Stand United, itakuwa kwenye Uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani kucheza na maafande wa Transit Camp yenye kumbukumbu mbaya baada ya kikosi hicho kuchapwa na Gunners FC kutoka Dodoma mabao 3-1.
Raundi ya 26 itahitimishwa kesho Jumapili kwa mechi moja kupigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma na Gunners iliyoichapa maafande wa Transit Camp mabao 3-1, itaikaribisha Stand United iliyotoka sare ya 1-1, dhidi ya Barberian FC.
Stand United ‘Chama la Wana’, ilishuka daraja msimu wa 2018-2019, ikimaliza nafasi ya 19 na pointi 44 baada ya timu hiyo yenye maskani yake huko Shinyanga kushinda mechi 12, ikitoka sare nane na kupoteza 18, ikifunga mabao 38 na kuruhusu 50.
Msimu uliopita, Stand ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu na pointi 61, ambapo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Off’ nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.
Kwa upande wa Fountain, ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29 katika Ligi Kuu msimu wa 2024-2025 na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza ya 13 na pointi 31, kwenye mechi ya mtoano na kikosi hicho cha maafande kushinda jumla ya mabao 4-2.