Simba Yamtema Mohamed Bajaber, Karabaka Apelekwa Mkopo Pamba Jiji
Klabu ya Simba imetangaza rasmi kufikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba wa kiungo mshambuliaji raia wa Kenya, Mohamed Bajaber.
Bajaber alijiunga na Msimbazi katika dirisha kubwa la usajili msimu wa 2025/2026 akitokea Kenya Police, lakini safari yake ndani ya klabu hiyo imegubikwa na changamoto za majeraha ya mara kwa mara yaliyomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Simba, klabu hiyo ilithibitisha:
“Kiungo mshambuliaji Mohamed Bajaber hatakuwa sehemu ya kikosi chetu kuelekea msimu mpya baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba. Uongozi wa klabu unamtakia kheri na baraka katika maisha yake mapya ya soka nje ya Simba.”
Saleh Karabaka Aelekea Pamba Jiji
Katika hatua nyingine, Simba imethibitisha kumtoa kwa mkopo wa msimu mmoja kiungo mshambuliaji Saleh Karabaka kwenda kuwatumikia Pamba Jiji.
Karabaka, aliyesajiliwa na Simba Januari 2024 akitokea JKU ya Zanzibar, amekuwa akitolewa kwa mkopo mara kwa mara ili kupata muda zaidi wa kucheza. Kabla ya kujiunga na JKT Tanzania msimu uliopita—ambapo aling’ara kwa kufunga mabao 8 ya Ligi Kuu ya NBC—pia aliwahi kucheza kwa mkopo ndani ya kikosi cha Namungo FC.