Ahmed Ally Afunguka: Kuondoka kwa Selemani Mwalimu Hakujaacha Pengo Simba
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kuweka wazi kuwa kuondoka kwa mshambuliaji Selemani Mwalimu hakujaleta pengo au kuathiri ufanisi wa safu yao ya ushambuliaji.
Ahmed amebainisha kuwa tangu kuondoka kwa Mwalimu, Simba SC imeendelea kuonyesha ukali wake katika kuzifumania nyavu kwenye kila mchezo iliyocheza, huku mara kadhaa ikiondoka na ushindi wa tofauti ya mabao mawili au zaidi.
“Haijawahi kuwa hasara kwa Simba kuondoka kwa Mwalimu. Hakuna mechi ambayo tumecheza na Simba haijapata goli. Tangu aondoke, kila mechi tunapata goli na mara nyingi tunashinda kwa zaidi ya bao moja,” alisema Ahmed Ally.
Ili kuthibitisha hilo, Ahmed alitolea mfano mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mighty Wanderers—ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0—huku michezo mingine yote ikiwa na wastani mzuri wa mabao ya kutosha.
Msemaji huyo aliongeza kuwa Mwalimu hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha kudumu, bali alikuwa akitumika kama chaguo la pili kulingana na mbinu za mwalimu.
“Katika kila mechi, ukiondoa mchezaji aliyekuwa kwenye mpango wa pili wa timu, huwezi kuvuruga mpango wa kwanza wa benchi la ufundi. Kwa maana hiyo, tuko salama na hakuna pengo la aina yoyote ndani ya kikosi,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Ahmed alikanusha vikali madai ya kuwepo kwa upendeleo wa wachezaji ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, akisisitiza kuwa nidhamu na viwango vya uwanjani ndivyo vinavyoamua nafasi ya mchezaji na wala si upendeleo.