Ahmed Ally: Azam FC Sio Nyonde, Simba Lazima Tutumie Akili Chamazi
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ametoa tahadhari kubwa kuelekea mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, akiwataka wachezaji wa Simba kuwa makini kwa dakika zote 90.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho kuikabili Azam FC katika mchezo unaotazamiwa kuwa wa ushindani na vuta-nikuvute kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Akizungumza kuelekea pambano hilo, Ahmed ameweka wazi kuwa Azam FC ni miongoni mwa timu zinazohitaji maandalizi ya hali ya juu kutokana na ubora wa kikosi chake na uwezo wa kubadilisha mchezo wakati wowote.
“Sio mpinzani nyonde nyonde, ni mpinzani ambaye anaweza kukupa mechi ngumu. Ni mpinzani ambaye ana wachezaji wenye uwezo wa kubadilisha mchezo hata uwe mgumu kiasi gani,” amesema Ahmed Ally.
Maboresho ya Azam FC na Ugumu wa Chamazi
Ahmed amebainisha kuwa maboresho yaliyofanywa na Azam msimu huu, pamoja na kurejea kwa baadhi ya nyota waliokuwa nje, yameongeza ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho. Pia alikiri kuwa kucheza ugenini katika Uwanja wa Azam Complex imekuwa changamoto ya kihistoria kwa Simba kupata matokeo kwa urahisi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Simba ina kikosi imara na morali ya juu ya kuondoka na pointi zote tatu.
Morali ya Ushindi wa Kimataifa (CAF)
Ushindi wa hivi karibuni dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi katika Ligi ya Mabingwa Afrika umeongeza kujiamini na nguvu mpya kikosini. Ahmed anaamini chini ya Kocha Mkuu Steve Barker, Simba itatumia vizuri nafasi zitakazopatikana ili kuondoka na ushindi.
“Kwa ubora tulionao Simba msimu huu, tunaamini tutaenda kupata matokeo mazuri. Ushindi wa kimataifa unatupa confidence kubwa na matumaini ya kuvuka kizingiti cha Azam Complex,” alihitimisha Ahmed.