Habari za michezo
BONUS ZA CAF ZATUA LIGI KUU KWA MASTAA WA YANGA
Vardo
May 23, 2026
9:49 am
KATIKA kuhakikisha anaongeza morali na hamasa ndani ya kikosi cha Yanga, mfadhili mkuu wa klabu hiyo, GSM, ameweka mezani dau kubwa la bonus kwa wachezaji kuelekea hatua za mwisho za msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa GSM amewaahidi mastaa wa Yanga kupewa bonus kubwa sawa na ile wanayopata katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika CAF kwa kila ushindi watakaoupata kwenye michezo iliyosalia ya ligi msimu huu.
Chanzo cha karibu ndani ya klabu hiyo kimesema lengo kubwa ni kuongeza ari ya ushindani kwa wachezaji ili kuhakikisha wanapambana mpaka mwisho katika mbio za kutetea ubingwa wa ligi kuu.
“Kuanzia sasa wachezaji wa Yanga watakuwa wanapata bonus sawa na ile ya mechi za CAF kwa kila ushindi wa michezo iliyobaki ya ligi. GSM anahitaji kuona ushindi pekee, si sare wala kupoteza, ili kuhakikisha timu inalitetea taji la ligi kuu msimu huu,” kilisema chanzo hicho.
Wakati huohuo, upande wa Simba nao umeendelea kuweka mazingira mazuri ya motisha kwa wachezaji wake, ambapo Rais wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ( MO Dewji) , hivi karibuni alifanya kikao na wachezaji pamoja na benchi la ufundi na kuwaahidi kuongeza bonus kadri timu inavyozidi kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Wachezaji wa Simba tayari wameanza kunufaika na mpango huo baada ya timu kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kufuatia ushindi walioupata dhidi ya TRA United katika hatua ya robo fainali