Wanaume 5 Wafikishwa Mahakamani Baada ya Kuendesha Gari la Maiti Uwanjani
NORTHUMBIA, ENGLAND — Ni tukio ambalo liliacha wengi vinywa wazi! Wanaume watano wameshtakiwa rasmi baada ya kufanya tukio la kushangaza la kuendesha gari la kubebea maiti pamoja na gari lingine hadi ndani ya uwanja wa mpira wa miguu na kufanya mizunguko iliyosababisha mchezo kusitishwa mara moja.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mbele ya maelfu ya mashabiki waliokuwa wakishuhudia mchezo wa maandalizi ya ligi ya daraja la chini nchini England, kati ya timu za Dunston UTS na Gateshead. Video za tukio hilo zilisambaa kwa kasi ya ajabu kwenye mitandao ya kijamii na kuzua gumzo kubwa duniani kote.
Katika tukio hilo, magari hayo mawili yalivunja vizuizi na kusimama katikati ya uwanja. Wanaume waliokuwa wamejifunika nyuso zao walitoka kwenye gari hilo la mazishi—lililokuwa na mabango mbalimbali madirishani—kisha kuingia kwenye gari jingine huku wakirusha vipeperushi uwanjani kabla ya kutokomea kwa kasi kwa gari aina ya Subaru.
Hati ya mashtaka inaeleza kuwa wanne kati ya watano hao walilazimisha kufunguliwa kwa mageti ya uwanja huo, na hivyo kuhatarisha maisha ya wachezaji na mashabiki waliokuwepo uwanjani. Mchezo huo ulisimama rasmi baada ya mapumziko ya kipindi cha kwanza huku timu zikiwa zimefungana bao 1-1.
Polisi wa Northumbria walithibitisha kuwafungulia mashtaka watuhumiwa hao watano na kuwafikisha katika Mahakama ya Hakimu ya Sunderland na South Tyneside.
Inspekta Mkuu wa Upelelezi, David Johnson, alieleza: “Tumekuwa tukifanyia kazi uchunguzi mrefu na tata tangu tulivyopata taarifa za tukio hili lenye mwelekeo wa kihalifu. Timu zetu zimefanya kazi usiku na mchana kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.”