Simba SC
JKT WAANGUSHWA, SIMBA QUEENS WAWEKA MKONO MMOJA KWENYE UBINGWA
Vardo
May 23, 2026
11:01 pm
SIMBA Queens wameendelea kuthibitisha ubora wao katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Queens katika mchezo uliopigwa leo Mei 23, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Simba Queens kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 52, huku wakitengeneza pengo la pointi 10 dhidi ya wapinzani wao wa karibu, JKT Queens na Yanga Princess ambao wote wamebaki na pointi 42.
Matokeo hayo yamewaweka Simba Queens katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa WPL msimu huu, kwani sasa wanahitaji ushindi katika michezo miwili pekee iliyosalia ili kuhakikisha taji linaendelea kubaki mikononi mwao.
Iwapo Simba Queens wataibuka na ushindi dhidi ya Tausi FC Mei 27 na kuifunga Mashujaa Queens Mei 31, watafikisha pointi 58 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu yoyote nyingine kwenye mbio za ubingwa.
Katika michezo mingine ya raundi ya 18 ya ligi hiyo, Yanga Princess walikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa Queens kwenye Uwanja wa TFF Kigamboni, huku Tausi FC wakiibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Ruangwa Queens. Nao Fountain Gate Princess waliwashinda Ceasiaa Queens mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa mkoani Manyara.
Kwa matokeo hayo, mashabiki wa Simba Queens wameanza kuhesabu mechi mbili pekee kabla ya kuanza rasmi sherehe za kutwaa ubingwa wa WPL msimu huu.